August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

eGA yaimarisha kilimo kupitia Mifumo ya Kidigitali

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

MAMLAKA  ya Serikali Mtandao (eGA) imesema inaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kujenga na kusimamia mifumo ya kidigitali inayorahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuboresha usimamizi wa shughuli za kilimo nchini.

Akizungumza leo Agosti 2,2026 na waandishi wa habari katika Maonesho ya  Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga, alisema mamlaka hiyo ipo kwenye maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake na mchango wake katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidigitali.


Kaswaga amesema eGA imepewa jukumu la kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya serikali ili kuhakikisha utendaji kazi wa taasisi za umma unafanyika kidigitali na huduma zote muhimu zinapatikana kwa wananchi kwa njia za kidigitali.


“Katika maonesho haya tunatoa elimu kwa wananchi ili wafahamu majukumu ya eGA na kuona hatua ambazo Tanzania inapiga katika matumizi ya teknolojia, sambamba na mabadiliko yanayoendelea duniani,” amesema.


Ameeleza kuwa katika sekta ya kilimo, eGA imeshirikiana na Wizara ya Kilimo kuunda mfumo wa eKilimo, unaowezesha serikali kupata taarifa sahihi za wakulima nchini, kurahisisha usimamizi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na utoaji wa vibali mbalimbali vya shughuli za kilimo.


Aidha, amesema mamlaka hiyo imeungana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutengeneza mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika unaowezesha shughuli zote za vyama hivyo kufanyika kidigitali huku ukiimarisha uwazi katika mauzo ya mazao na malipo kwa wakulima.


“Kupitia mfumo huu, mkulima anaweza kufuatilia mauzo ya mazao yake, kujua kiasi kilichouzwa na mapato anayostahili kupata,mumo umeongeza uwazi na uwajibikaji katika vyama vya ushirika,” amesema.


Kaswaga amesema hadi sasa zaidi ya vyama 6,000 vya ushirika vimesajiliwa kwenye mfumo huo, ambao pia unasaidia kudhibiti upotevu wa mapato.


Kwa upande wa pembejeo, Kaswaga amesema eGA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imejenga Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea (Fertilizer Information System – FIS), unaowezesha kusimamia wazalishaji na waagizaji wa mbolea, kufuatilia mwenendo wa soko na kuhakikisha bei elekezi za serikali zinazingatiwa.


Amesema mfumo huo umeiwezesha serikali kudhibiti soko la mbolea na kuwasaidia wakulima kupata mbolea kwa bei elekezi, hatua inayochangia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.


Kaswaga ameongeza kuwa eGA itaendelea kushirikiana na sekta ya kilimo pamoja na taasisi nyingine za serikali katika kuendeleza matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidigitali, ikiwemo mfumo wa barua pepe za serikali na Ofisi Mtandao, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa serikali.