October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taarifa sahihi ,Teknolojia kuwezesha wachimbaji wadogo



Na Joyce Kasiki, Geita


WADAU wa sekta ya madini wamezitaka kampuni kubwa za uchimbaji na taasisi zinazohusika na sekta hiyo kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata teknolojia, vifaa na taarifa sahihi za kijiolojia ili kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.


Wito huo umetolewa mkoani Geita wakati wa maonesho ya madini, ambapo viongozi wa sekta hiyo wamesema upatikanaji wa taarifa sahihi za maeneo yenye viashiria vya madini unaweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya maamuzi kwa kuzingatia utafiti badala ya kubahatisha.


Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji, John Bina Wambura, amesema ushirikiano kati ya kampuni kubwa za uchimbaji na wachimbaji wadogo ni muhimu katika kuwaongezea ujuzi na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa.


Amesema hatua hiyo inaweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama na kupanua shughuli zao, hali ambayo inaweza kuwawezesha kukua kutoka kiwango cha uchimbaji mdogo hadi kuwa wachimbaji wakubwa.


Mwenyekiti wa Wachimba Madini Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Dhahabu Taifa, Titus Charles Kabuo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano huo, akieleza kuwa utaalamu na teknolojia kutoka kwa kampuni kubwa unaweza kusaidia kuboresha namna wachimbaji wadogo wanavyoendesha shughuli zao.


Kwa upande mwingine, viongozi hao wameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuimarisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na machapisho yanayoonesha maeneo yenye viashiria vya madini.


Wamesema taarifa hizo zitawasaidia wachimbaji kupanga shughuli zao kwa ufanisi na kupunguza uwezekano wa kutumia fedha na rasilimali katika maeneo yasiyo na matokeo yanayotarajiwa.


Mwenyekiti wa Wanawake Wachimbaji Mkoa wa Geita, Evelyn Clofas Nzinza, amesema upatikanaji wa vifaa bora na vinavyokidhi mahitaji ya wachimbaji kwa gharama nafuu ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji.


Ameeleza pia umuhimu wa kuunga mkono kampuni zinazowezesha wachimbaji kupata vifaa kwa bei rafiki, ikiwemo Kerama, ili kuongeza upatikanaji wa zana zinazoweza kukidhi mahitaji ya shughuli zao.


Viongozi hao wamesema maendeleo ya sekta ya madini yanahitaji ushirikiano kati ya serikali, taasisi za utafiti, kampuni kubwa za uchimbaji na wachimbaji wadogo.


Aidha, wamesisitiza umuhimu wa wadau wa sekta hiyo kuzingatia sheria na kutimiza wajibu wa kulipa kodi stahiki, wakieleza kuwa hatua hizo zinaweza kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha mchango wa madini katika uchumi wa taifa.


Kwa mujibu wa viongozi hao, uwezeshaji wa wachimbaji wadogo kupitia teknolojia, taarifa sahihi za utafiti, vifaa bora na ujuzi wa kitaalamu ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kujenga sekta ya madini yenye tija na kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.