October 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 90 fedha sekta ya madini kubaki nchini


Na Joyce Kasiki,Geita

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 90 ya shilingi trilioni 5.1 zinazotumika kila mwaka kununua bidhaa na huduma katika sekta ya madini zinabaki nchini.


Mavunde amesema hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa Sera ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.


Waziri huyo ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya Siku ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, mkoani Geita, sambamba na Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Geita.


Amesema fursa za kiuchumi katika sekta hiyo zinatarajiwa kuongezeka kutokana na kampuni 14 zinazotarajiwa kuanzisha miradi mikubwa ya madini, pamoja na leseni 28 za uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite), ambazo Serikali imekuwa ikizitaka zianze uzalishaji.


Mavunde amezitaka kampuni za Kitanzania kujiandaa mapema kwa kuunganisha mitaji, teknolojia, utaalamu na uzoefu ili kuongeza uwezo wa kushiriki katika fursa zinazotokana na miradi hiyo.


Amesema kampuni hizo hazipaswi kusubiri miradi ianze ndipo zijenge uwezo, bali zinapaswa kuanza maandalizi sasa ili kuhakikisha zinakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.


Kwa sasa, kati ya ajira rasmi zaidi ya 19,000 katika sekta ya madini, asilimia 96 zinashikiliwa na Watanzania, huku idadi ya kampuni za Kitanzania zinazoshiriki katika mnyororo wa ugavi ikiendelea kuongezeka.


Kwa upande wake, Rais wa Wachimbaji Wadogo, John Bina, ameishukuru Serikali kwa namna ilivyoendelea kuwaunga mkono wachimbaji hao na kuwapa umuhimu katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.