


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amelipongeza Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kwa hatua kubwa linazopiga katika kuendeleza sekta ya uvuvi, akisisitiza kuwa ni sekta ya kimkakati inayopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo leo Agosti 1, 2026, alipotembelea banda la TAFICO katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji maarufu kama Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.
Amesema dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uvuvi imeonekana kwa vitendo kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika ujenzi wa bandari za uvuvi pamoja na ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa, hatua zitakazowezesha uvuvi wa bahari kuu na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
“Hongera TAFICO,hii ni sekta ya kimkakati na dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuiinua imeonekana kwa vitendo kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika.”amesema Dkt.Nchemba na kuongeza kuwa
” Endeleeni kusonga mbele, nasi tutaendelea kuimarisha miundombinu ya bandari ili kuwezesha kufikia maeneo ya kina kirefu kwa shughuli za uvuvi,” alisema Waziri Mkuu.”
Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko, Zalisha kwa Tija Kutekeleza Dira ya 2050.
Akitoa maelezo kuhusu shughuli za shirika hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa, amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya uvuvi kwa kuimarisha uwezo wa shirika kupitia ununuzi wa meli za kisasa na ujenzi wa bandari maalumu za uvuvi.
Amesema uwekezaji huo utachochea ukuaji wa uchumi wa bluu kwa kuongeza ajira, kuboresha huduma za uhifadhi na usafirishaji wa mazao ya uvuvi pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
“Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania kwa kuhakikisha linapata meli za kisasa za uvuvi wa bahari kuu na kujenga bandari ambazo zitakuwa kitovu cha shughuli za uvuvi. Hivi sasa TAFICO ina meli moja inayotekeleza shughuli za uvuvi wa bahari kuu na tunaendelea kukamilisha taratibu za kuongeza nyingine,” amesema Matessa.
Ameongeza kuwa Serikali inatarajia kununua meli nyingine nne kwa awamu, ambapo mbili zinatarajiwa kupatikana katika kipindi cha karibu, hatua itakayoongeza uwezo wa shirika kuvua katika maeneo ya Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) ambayo hayajatumika ipasavyo kwa miaka mingi.
Matessa amesema TAFICO itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika shughuli za uvuvi wa bahari kuu ili kuongeza tija na kuhakikisha rasilimali za bahari zinachangia zaidi maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Amemshukuru Waziri Mkuu kwa kutembelea banda la shirika hilo na kuahidi kuwa TAFICO itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha mazao ya uvuvi yanatumika kwa tija, yanazalisha ajira, yanaongeza mapato ya Serikali na kuvutia wawekezaji katika Uchumi wa Bluu.

More Stories
TVLA yaonya homa ya kutupa mimba mifugoni
Mwigulu ataka huduma za TPHPA ziwafikie wakulima wengi
Nchemba aipongeza TPHPA Kwa huduma bora