Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu, amewataka wakulima na wadau wa sekta ya kilimo nchini kutumia mbegu zilizoidhinishwa na kuthibitishwa na TOSCI ili kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa mazao katika soko la ndani na kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TOSCI kwenye Maonyesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Chimagu amesema mbegu bora ndiyo msingi wa mapinduzi ya kilimo na utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka huu inayohamasisha uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko.
Amesema TOSCI imejipanga kutumia maonyesho hayo kutoa elimu kwa wakulima, wazalishaji wa mbegu na wafanyabiashara kuhusu uzalishaji, usajili, usafirishaji na biashara ya mbegu bora, ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
“Tunatoa mafunzo kwa wote wanaotaka kujihusisha na uzalishaji na biashara ya mbegu. Mbegu ni biashara yenye fursa kubwa, hivyo ni muhimu wadau wapate elimu na vyeti vinavyowawezesha kufanya shughuli hizo kwa kuzingatia sheria na viwango vya ubora,” amesema Chimagu.
Alieleza kuwa TOSCI pia inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu namna ya kutambua mbegu halisi zilizothibitishwa kwa kutumia lebo maalumu za uthibitisho pamoja na mfumo wa kielektroniki unaomwezesha mkulima kuhakiki ubora wa mbegu kupitia simu ya mkononi kwa kupiga 14852# na kufuata maelekezo.
Chimagu amesema katika mabanda ya maonyesho, TOSCI imeanzisha mashamba darasa yanayoonesha tofauti kati ya matumizi ya mbegu bora na zisizo bora, akieleza kuwa matumizi ya mbegu zilizoidhinishwa yanaweza kuongeza uzalishaji wa mahindi kutoka wastani wa tani 2.1 kwa hekta hadi tani tano hadi 10 kwa hekta endapo mkulima atafuata kanuni bora za kilimo.
Amesema taasisi hiyo pia imejikita katika kuhakikisha wakulima wanapata miche bora ya mazao mbalimbali ikiwemo parachichi, huku aina tano za miche hiyo tayari zikiwa zimeidhinishwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Tunawaomba wakulima na wadau wote wa kilimo kutembelea banda la TOSCI hapa Nzuguni na katika kanda zote nchini ili wapate elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora, fursa za uzalishaji wa mbegu na namna ya kuanzisha biashara ya mbegu zenye ubora uliothibitishwa,” amesema.
Ameongeza kuwa TOSCI inaendelea kuwaunganisha wazalishaji wa mbegu na taasisi za kifedha ili kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha au kupanua shughuli za uzalishaji na biashara ya mbegu bora, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mbegu zenye ubora na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

More Stories
BRELA yatahadharisha dhidi ya matumizi holela ya majina
TVLA yaonya homa ya kutupa mimba mifugoni
Waziri Mkuu Aipongeza TAFICO kwa mafanikio Nanenane