June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa masoko watakiwa kufuata Sheria

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

VIONGOZI 19 wa soko la Kiloleli na Mwaloni Kirumba  wilayani Ilemela mkoani Mwanza waliochaguliwa  hivi karibuni,wamekula kiapo cha uadilifu ili kuongoza masoko hayo kwa kipindi cha miaka mitatu wakiwemo Wenyeviti, Makatibu na Wahasibu.

Akiongoza kiapo hicho Juni 2,2026,Mwanasheria wa Serikali Wakili Kanisia Ngutu, aliwataka viongozi hao kufuata sheria , kanuni na taratibu katika kuongoza na kutatua changamoto za wafanyabiashara.

Amesema viongozi hao ni kiungo kati ya wafanyabiashara na Serikali hivyo aliwataka kulinda na kutii kiapo walichoapa kwani kwenda kinyume ni kuvunja sheria na hatua  zitachukuliwa dhidi yao.

Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Kefa Gembe,amewataka viongozi  hao viongozi kuwa daraja zuri  ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli za uzalishaji mali   kwa amani ili halmashauri iweze mapato ambayo yatatumika  kuwaletea wananchi maendeleo.

Mwenyekiti soko la Mwaloni Kirumba Fikiri Mzinza,ameishukuru Serikali kwa miongozo na maelekezo waliowapatia na kuahidi kwenda kuwa kiunganishi sahihi kwa wafanyabiashara.

Huku Mwenyekiti soko la Kiloleli Mashimba Mabula,ameomba ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wafanyabiashara uendelee ili  kukuza biashara,mazingira mazuri na  kuimarisha uchumi wa wananchi.