June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi akagua jengo la dharura la Bil,1.6


Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Manyara.

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amesema hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya afya ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya “Kazi na Utu” inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo yao.

Kihongosi ameyasema hayo leo Juni 2, 2026 alipokua akikagua jengo la dharura (Emergency) la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, miradi iliyotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. Bil 1.6.

Amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuimarisha huduma za afya na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi waliolazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ya kibingwa.

“Tumepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huu na tumekagua majengo mawili muhimu sana, Jengo la Dharura pamoja na Jengo la ICU. Miradi hii imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.6 ambazo zimetolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi,” amesema Kihongosi.

Aidha, amepongeza ubora wa kazi zilizotekelezwa pamoja na usimamizi mzuri uliofanywa na viongozi wa mkoa na wataalamu wa afya waliohusika katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kazi iliyofanyika hapa ni ya kiwango cha juu na inaakisi dhamira ya Serikali ya CCM ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika mazingira rafiki na salama,” amesema.

Ameeleza kuwa hapo awali wananchi wengi wa Mkoa wa Manyara walilazimika kwenda katika hospitali za rufaa na kibingwa zilizoko nje ya mkoa huo kwa ajili ya kupata huduma maalumu za matibabu, lakini sasa hali hiyo inaendelea kupungua kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu ya afya.

“Miaka iliyopita wananchi walilazimika kwenda KCMC au Muhimbili kupata baadhi ya huduma za matibabu. Leo hii huduma nyingi muhimu zinapatikana hapa hapa Manyara. Huu ni utekelezaji wa kweli wa falsafa ya Kazi na Utu kwa kuwa huduma zinamfikia mwananchi badala ya mwananchi kuendelea kuzifuata mbali,” amesema.

Kihongosi pia ameipongeza hospitali hiyo kwa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine ya CT Scan pamoja na huduma nyingine zinazoongeza ufanisi katika utoaji wa matibabu.

Vilevile, ameonesha kufurahishwa na uwepo wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba (oxygen plant) ambao umeongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wanaohitaji oksijeni.

“Awali hospitali haikuwa na mtambo wa kuzalisha oksijeni, lakini sasa huduma hiyo inapatikana hapa. Zaidi ya hapo, mfumo wa kusambaza oksijeni moja kwa moja katika vyumba vya wagonjwa umewekwa, jambo linalorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza usalama kwa wagonjwa,” amesema.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wananchi pamoja na watumishi wa hospitali kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

“Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miradi hii inalindwa. Fedha nyingi zimewekezwa na ikiharibiwa ni wananchi wenyewe watakaopoteza manufaa yake. Tuitunze ili iendelee kuhudumia kizazi cha sasa na vijavyo,” amesema.