April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JIKOKOA watoa ombi kwa serikali

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Watengenezaji wa jiko la kuni na mkaa ambalo hutumia mkaa na kuni kidogo kwa matumizi makubwa ya nyumbani (Jikokoa) wameiomba serikali kupunguza masharti ambayo wameyaweka kwani majiko hayo wanayalipia ushuru mkubwa ambapo ikitokea wanapandisha bei, watumiaji wa majikohayo watashindwa kununua na kuweza kufanya shughuli zao kwa urahisi.

Hayo aliyasema Mkurugenzi wa Biashara Afrika Mashariki, Irene Kamande wakati wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia ‘Tanzania Clean Cooking, Conference’ lililofanyika , katika ukumbi wa mikutano JNICC, jijini Dar es Salaam.

Kamande alisema walianza kufanya utafiti miaka kadhaa iliyopita wakaona kuna utumizi mkubwa sana wa mkaa na ambapo wakaleta majiko hayo ili kumsaidia mwananchi kuweza kuendesha maisha yake kwa urahisi bila madhara yoyote ikiwemo kupata madhara mwilini au kifo.

Kamande alisema majiko yao yanatumia mkaa na kuni chache na hayana madhara kwa mtumiaji kwasababu hewa mbaya ambayo inatoka ni ndogo tofauti na ile ambayo inatoka kwenye jiko la kawaida

Alisema Majiko yao yanapatikana kwa bei ya chini ambayo kila mtanzania anaweza nunua lakini pia yanatumia mkaa mdogo sana ambapo kwa mwezi mtu anaweza kutumia gunia zima lakini kwa kutumia majiko hayo mtu atatumia 30% tu ya mkaa.

“Kwa sasa tumeweka bei ambayo imesaidia kuongeza soko kwa kuuza majiko kwa wingi, ambapo tumesambaza majiko katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha na kwa sasa tupo Dar ambapo Mbeya na Mwanza tutafika pia”

Kuhusu kuongeza Ajira kupitia biashara hiyo, Kamande alisema wameajiri watu zaidi ya 100 na mpaka kufikia mwaka 2023 wanampango wa kuongeza ajira kwa watu takribani 2000.

“Jiko okoa imesaidia sana kuongeza fursa za ajira na sasa tumeshaajiri watu takribani 100 na hadi kufikia mwezi Disemba tutakua tumeajiri watu zaidi ya 500 na matarajio yetu hadi kufikia mwaka mmoja ujao tutaajiri watu 2000”

Aidha aliwataka Wananchi kutumia jikokoa kwani litaokoa pesa na afya.