April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bashe-Tanzania inahitaji alama ya biashara ya kipekee kutambulisha bidhaa za kilimo nje ya nchi

Na Penina Malundo,timesmajira

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema imefika wakati sasa kwa Taasisi zinazohusika na masuala ya Miliki Ubunifu kuja na mapendekezo yatakayowezesha Tanzania kuwa na alama ya biashara ya kipekee itakayotambulisha bidhaa za Tanzania duniani kote.

Waziri Bashe ametoa rai hiyo leo jijini Dodoma alipotembelewa ofisini kwake na ujumbe kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO) ambalo makao makuu yake yako Harare- Zimbabwe, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shrikika hilo Bemanya Twebaze, aliyeambatana na Mwenyeji wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa.

Bashe amesema Tanzania ikiwa na alama yake ya biashara ya kipekee mfano kwa bidhaa zake zote za kilimo zinazouzwa nje ya nchi itawezesha kutambulika duniani kote na thamani ya bidhaa hizo kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi zinauzwa nje ya nchi lakini hazitambuliki kama bidhaa za Tanzania kama nchi.
Pia kutumika kwa Alama ya Tanzania kutazitangaza bidhaa za kilimo kutoka Tanzania. Hii itasaidia kujua mnyororo wa thamani wa bidhaa zote za kilimo.

“Ukiangalia bidhaa ya Champagne ni mvinyo unajulikana duniani kote kutokana jina la mahali bidhaa hiyo ilikozalishwa kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa, Ifike wakati sasa bidhaa za Tanzania zijulikane kwa alama ya kipekee duniani kote”, amesisitiza Bashe.

Akizungumzia Ufadhili wa wanafunzi watano kila mwaka wanaosomea Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya ufadhili wa BRELA, wakati ARIPO ikitoa utaalam wa kiufundi na ufadhili, ameshauri pia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC) pia zijumuishwe kwenye mpango huo kwani vumbuzi nyingi zinafanyika katika taasisi hizo hivyo ni vyema zikawezeshwa zaidi.

Bashe amesema katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na ARIPO za kuendeleza Miliki Ubunifu kwa nchi wananchama wa ARIPO wizara yake itaridhia Itifaki ya Arusha inayohusu ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea iliyosainiwa Arusha mwaka 2015 na kuelekeza viongozi wa Wizara ya Kilimo kuanza mchakato wa kuridhiwa kwa Itifaki ya Arusha, kwani haileti picha nzuri kwa kutoridhia Itifaki iliyosainiwa mwaka 2015 Mkoani Arusha.

Awali akimtambulisha, Twebaze, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Nyaisa amesema BRELA ikiwa ni miongoni mwa wanachama wa ARIPO imekuwa ikinufaika na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Shirika hilo ya kuwajengea uwezo watumishi wa BRELA, Nyaisa amesema BRELA inatambua umuhimu wa Miliki Ubunifu kwa Tanzania ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele kutoa ufadhali wa masomo kwa Watanzania ili wawe chachu katika kuhakikisha kuwa wabunifu wananufaika na bunifu zao na kulindwa kisheria.

Kwa upande wake, Twebaze ameshukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao ARIPO inaupata kupitia BRELA kwani ujumbe huu ukiwa nchini Tanzania umekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya Umma zinazojihusisha na masuala ya Ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea chini ya Itifaki ya Arusha ambayo inasubiri kuridhiwa.

Amesema pia baada ya kufanya ziara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzungumza na uongozi wa chuo hicho ameridhishwa na mashirikiano yaliyopo kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
BRELA katika kufanikisha ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi ambao wanatoka nchi wanachama wa ARIPO ikiwemo Tanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uwekezaj, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amepokutana na ujumbe huo wa ARIPO katika ofisi za BRELA jijini Dodoma, ameahidi wizara yake kufuatilia kwa karibu ili Itifaki ya Arusha iridhiwe mapema na kuanza kutumika ambayo itawezesha upatikanaji wa mbegu na uzalishaji wa chakula cha kutosha kutokana na ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea.

“Itifaki hii ni muhimu na itaridhiwa mapema iwezekanavyo kwani nchi inahitaji kujitosheleza kwa chakula hivyo ni vyema bunifu hizi zikalindwa ikiwa ni pamoja na wahusika kunufaika”, amesisitiza Kigahe.

Ujumbe wa ARIPO ambao umeondoka jana kurejea nchini Zimbabwe umekuwepo nchini kwa siku nne na mbali ya kukutana na viongozi pamoja na wadau, pia ulipata fursa ya kutembelea mji wa Serikali wa Magufuli uliopo Mtumba jijini Dodoma, pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa ambapo Twebaze amepongeza maendeleo yanayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.