August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIRC yatangaza neema kwa Wakulima Nanenane

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), inaendelea na utekelezaji wa Mkakati mkubwa wa kuimarisha kilimo cha Umwagiliaji
nchini kwa kuzindua miradi mipya zaidi ya 30 katika mwaka wa fedha 2026/27, huku ikitarajia kuajiri maelfu ya vijana kupitia uchimbaji wa visima na usimamizi wa miundombinu ya Umwagiliaji.

Pia inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kufanikisha azma ya sekta ya kilimo kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dr. John Malecela, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema kwa kipindi cha miaka michache ya utekelezaji wa majukumu yake, tume imefanikiwa kuwa na wakandarasi 146 wanaotekeleza miradi mbalimbali ya Umwagiliaji, huku miradi 634 ikiwa katika hatua za usanifu.

Amesema lengo ni kuhakikisha mkulima anakuwa na uwezo wa kuzalisha kwa tija na kuacha kutegemea mvua.

“Tume inatarajia kuanza zoezi kubwa la kugawa pampu za maji katika mikoa saba nchini, ambapo zoezi hili litaanza rasmi mkoani Katavi ifikapo tarehe 11,”amesema

Katika mpango huo, jumla ya pampu za kawaida (surface pumps) 1,000 zitatolewa ili kuwasaidia wakulima wa mbogamboga na matunda kuvuta maji kwa urahisi kutoka kwenye mito na mabonde, jambo ambalo litafanyika kwa njia salama isiyoharibu mazingira.

Sambamba na hilo, zaidi ya pampu 1,000 za kisasa zinazotumia nishati ya jua (solar pumps) zimenunuliwa maalum kwa ajili ya wakulima wa zao la parachichi.

“Wakulima hawa mara nyingi hukumbana na changamoto ya miinuko na mabonde inayokwamisha mifumo ya kawaida ya Umwagiliaji, hivyo pampu hizi ni mkombozi wao mkuu

Ameongeza kuwa “Habari njema zaidi inawaendea vijana mtaani kwani Tume imebuni mradi mkubwa wa uchimbaji wa visima ambao unalenga kuajiri kati ya vijana 2,000 hadi 4,000 ndani ya miaka mitatu ijayo,amesisitiza

Amesema,Mpango huo utahusisha kuunda katika vikundi vijana wenye ujuzi wa ufundi na uhandisi kwenye halmashauri zote 184 nchini.

Aidha Tume itawawezesha vijana hawa kusimamia miradi hiyo na kufunga miundombinu ya visima kwenye maeneo yao badala ya kusubiri waajiriwa kutoka nje.

Mpaka sasa, tayari visima 415 vimechimbwa huku lengo kuu likiwa ni kuchimba visima 67,000 ndani ya miaka nane ijayo.

Akifafanua zaidi kuhusu kazi zinazoendelea, Mkurugenzi Mndolwa amesema Tume imefanikiwa kusimamia mikataba 146 ya ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji ambapo wakandarasi wapo kazini.

Zaidi ya miradi 634 ipo katika hatua za usanifu na katika mwaka wa fedha 2026/2027, miradi mipya 30 inatarajiwa kuzinduliwa.