Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online,Mara.
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama mkoani Mara imetakiwa kuendelea kuhimiza wazazi na walezi kuimarisha malezi bora kwa watoto ili kuandaa kizazi chenye maadili na uzalendo.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 4, 2026 na Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya UWT Wilaya ya Butiama yaliyofanyika Kata ya Kukirango wilayani Butiama.

Maadhimisho hayo, yameenda sambamba na kuchangia ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT Wilaya ya Butiama inayojengwa katika kata hiyo, ambayo kwa sasa ipo katika hatua ya upauaji.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Samwelly amesema,UWT ina wajibu wa kuhakikisha wazazi na walezi wanasimamia maadili na malezi bora ya watoto ili Taifa liwe na watu wema ambao pia watashiriki katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Rhobi ameitala UWT kuendelea kushirikiana na kushikamana katika masuala mbalimbali ya maendeleo ndani ya jumuiya na chama hicho kwa ujumla.
“Ushirikiano utaendelea kuifanya jumuiya kupiga hatua mbalimbali, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Katibu. Pia utaendelea kukifanya chama chetu kizidi kuwa imara katika kushika dola na kuwatumikia Watanzania kwa kuwaletea maendeleo,” amesema Samwelly.
Hata hivyo amewataka wananchi kuwakemea wanaohubiri chuki, mafarakano na utengano miongoni mwa Watanzania, akisisitiza kuwa watu hao hawana nia njema na Taifa.
“Tuwakemee wale wanaohubiri chuki, mafarakano na utengano miongoni mwa Watanzania kwani hawana nia njema. Toeni taarifa mapema mnapoona watu wanataka kuleta uvunjifu wa amani katika maeneo yenu ili amani iliyopo iendelee kudumishwa,” amesema.
Katika kufanikisha ukamilishaji wa nyumba hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Christopher Marwa, amechangia sh.500,000, huku Mbunge wa Butiama, Dkt. Charles Mahera, akichangia sh. 500,000 pamoja na mbao za kuezekea jengo hilo huku Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly, ameahidi kuchangia fedha ili kufanikisha upauaji huo.

Awali, Katibu wa UWT Wilaya ya Butiama, Ester Tuma, akisoma taarifa ya ujenzi amesema,ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2023 katika Kata ya Kukirango ukiwezeshwa na viongozi wa jumuiya hiyo Wilaya ya Butiama na viongozi wa CCM.
Amesema, hadi sasa ujenzi huo umegharimu zaidi ya sh.mil. 15, ambapo jengo lipo katika hatua ya upauaji, na ujenzi wote unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh.52.4.

More Stories
Uwekezaji wa Michezo wavutia Watalii Tanzania
Mkurugenzi Bonde Rufiji, ahimiza utunzaji vyanzo vya maji
DC Nkasi na kampeni ya mjue jirani yako kuimarisha usalama