Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
TAASISI ya Utafiti Tanzania (TARI) kituo cha Ukiriguru imepiga hatua katika tafiti za mazao ya mizizi, hususani mihogo na viazi vitamu, kwa kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mbegu bora na kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Akizungumza Agosti 2,2026 kwenye banda la taasisi hiyo katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayoendelea viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Mtafiti kutoa TARI kituo cha Ukiriguru Mwanjia Ngangambe amesema,taasisi hiyo ina jukumu la kufanya tafiti mbalimbali na kituo cha Ukiriguru wana mamlaka ya kufanya utafiti wa mazao mawili ya pamba na mazao ya mizizi ya mihogo na viazi.

Ambapo amesema,kupitia kituo cha Ukiriguru kwa zao la pamba wamefanikiwa kugundua aina tano za mbegu bora,lakini ipo mbegu moja ya UKM08 ambayo ina mavuno ya kutosha,inavumilia magonjwa lakini pia inalimwa nchi nzima kwa mikoa ambayo inalima zao hilo.
“Kupitia kitengo cha pamba tumeweza kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na magonjwa pamoja na wadudu ambazo ni mbinu husishi,kama tunavyojua hivi sasa wakulima wengi wanatumia viuatilifu kwa muda mrefu na kusababisha mdudu kutengeneza usugu na ile dawa kutokufanya vizuri,”amesema Ngangambe.
Ngangambe amesema,katika mazao ya mizizi wamefanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na mifumo ya mbegu kwenye mihogo pamoja na viazi vitamu.Kwa upande wa mihongo kuanzia mwaka 2005 waliweza kugundua takribani aina 27 za mbegu bora ambazo mkulima akipanda anapata tija
Pia amesema,wameweza kuimarisha mifumo ya mbegu ya mazao ya mizizi kwa sababu mazao hayo yalikuwa hayana mifumo rasmi ya mbegu,ambapo mkulima akitaka mahindi atapata mbegu kwenye duka la pembejeo lakini akitaka mbegu ya muhogo hawezi kuipata.
“Tumeweza kuanzisha chama cha wazalishaji wa mbegu Kanda ya Ziwa kupitia mihogo na viazi.Hayo kwetu ni mafanikio ukiangazia kwenye viazi vitamu tumeweza kugundua takribani aina 20 za mbegu za viazi vitamu na kati ya mbegu hizo kuna zaidi ya aina 10 za mbegu za viazi lishe ambavyo vina vitamini “A” ya kutosha ambayo ina umuhimu kwenye mwili wa binadamu na kwani inaongeza kinga ya mwili, kuimarisha afya ya macho na kupunguza tatizo la utapia mlo,”amesema Ngangambe.
Sanjari na hayo amesema,mbali na kugundua mbegu mpya, taasisi hiyo imeboresha takribani aina nane za mbegu za asili zilizokuwa zikitumiwa na wakulima na kuzithibitisha kupitia Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI),miongoni mwa mbegu hizo ni aina za Ukerewe na Polista.

Hata hivyo amesema, taasisi hiyo inaendelea kuwashauri wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo na kutumia teknolojia zilizofanyiwa utafiti ili kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani huku akitolea mfano kupitia zao la pamba linaweza kutumika kuzalisha mafuta na malighafi za nguo, huku mihogo na viazi vitamu vikitumika kutengeneza keki,”chripsi” na unga wa muhogo.
Vilevile amesema,mkulima wa pamba anayezingatia teknolojia ambazo taasisi hiyo imezigundua na kuzizalisha pamoja na kanuni bora za kilimo ana uwezo wa kuvuna zaidi ya kilo 1,000 kwa ekari. Mafanikio hayo yanatokana na ubunifu wa teknolojia mpya ikiwemo nafasi bora ya upandaji ambayo imeongeza uzalishaji.
Kadhalika alitoa wito kwa halmashauri na Maofisa Ugani kuwafundisha wakulima teknolojia zilizobuniwa na taasisi hiyo , huku akiwahimiza wakulima kujifunza na kuzitumia ili kuongeza uzalishaji, kipato na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.


More Stories
EWURA yahamasisha uwekezaji vituo vya mafuta vijijini
NIRC yatangaza neema kwa Wakulima Nanenane
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi