April 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa(CFR), Dkt.Jeremia Ponera (kulia) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jijini Dar es salaam, kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa chuo hicho ikiwemo kujitanua na kuwafikia Watanzania wengi zaidi sambamba na kuongeza programu na kozi mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025. Picha na mpiga picha wetu.

Chuo cha Diplomsia kutumia bil.12/- kujipanua

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR) cha Jijini Dar es
Salaam kinatarajia kutumia sh. bilioni 12 kwa ajili ya kujipanua ikiwemo ujenzi wa majengo mapya na kuanzisha kampasi mpya mikoani ili kuongeza idadi wanufaika wa programu na kozi zinazotolewa na chuo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Mkurugenzi wa Chuo hiyo, Dkt. Jeremia Ponera amesema kujipanua kwa
chuo kunakwenda sambamba na kuongeza programu na kozi mbalimbali ili
kukidhi matakwa na mahitaji ya soko la ajira hapa nchini.

“Tunapenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.
John Magufuli kwa kutenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa chuo
hiki.

Tutajenga vyumba vya mihadhara, maabara ya lugha, maktaba ya
kisasa, vyumba vidogo vya kufundishia na semina, hosteli za wanafunzi
pamoja na maeneo ya kujifunzia,” amesema Dkt. Ponera.

Dkt. Ponera alisema mradi wa upanuzi wa chuo utasaidia kuongeza idadi
ya wanafunzi kutoka 1,500 hadi kupifikia wanafunzi 4,000 kwa Dar es
Salaam peke yake.

“Tunarajia kufungua kampasi tatu Dodoma, Arusha na Zanzibar ilikupanua
wigo na kutoa fursa kwa Watanzania wengi wenye kiu ya kujiunga na
programu pamoja na kozi mbalimbali waweze kufikiwa kwa
haraka,”amesema.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo elimu inayotolewa na
CFR itakuwa imewafikia Watanzania wengi mikoani ambao walikuwa
wanalazimika kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na programu na
kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo.

“Tumeshafika Dodoma na tupo katika hatua za mwisho za kupata ardhi na
kuanza ujenzi na tunategemea katika kipindi cha miaka mitatu ijayo
tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa kampasi yako,” amesema Dkt. Ponera na
kuongeza kuwa Chuo kimeshapata pia kiwanja katika mkoa wa Arusha.

Amesema CFR kimejipanga kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025, sambamba na
kujenga ufahamu, kuvutia uwekezaji na biashara za kimataifa.

“Chuo cha Diplomasia kinaandaa na kutoa mafunzo kutokana na uhitaji
mbalimbali katika jamii,” amesema na kuongeza kuwa chuo chake ni hazina kubwa ya maarifa katika nyanja za diplomasia na uhusiano wa
kimataifa.

Kwa upande wake, Mrajisi (Registrar) wa Chuo hicho, Dkt. Ally Masabo
alisema chuo kwa sasa kinatoa program za Astashada, Stashada, Shahada
na Shahada za Uzamili katika nyanja mbalimbali.

“Tunazo pia kozi fupi fupi ambazo mtu yeyote anaweza kujiunga kwani
hazihitaji sifa za kujiunga. Tunawakaribisha Watanzania kuja
kutembelea na kujifunza kozi mbalimbali ili kujiongezea maarifa,”
amesema Dkt. Masabo.

Kituo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa kilianzishwa mwaka 1978
kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Msumbiji. Kimepewa jukumu la kuwaandaa Watanzania katika mafunzo ya
diplomasia, lugha, stratejia na diplomasia za kiuchumi.