May 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa. (Picha na Maktaba).

Vijiji vyote kufikiwa umeme-Majaliwa

Vijiji vyote kufikiwa umeme-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vijiji 25 vya wilaya ya Ruangwa ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi walio katika vijiji ambavyo bado havijaunganishiwa nishati ya umeme wafanye maandalizi kwa sababu maeneo mengine tayari wakandarasi wameshapatikana.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wakati alipozungumza na wananchi katika vijiji vya Nanjaru, Nambilanje, Mkaranga, Namichiga na Mbekenyera akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema wilaya ya Ruangwa ina jumla ya vijiji 90 kati yake vijiji 25 tu ndio bado havijafikiwa na huduma ya umeme lakini tayari mkandarasi ameshapatikana na ameshaanza kazi, hivyo aliwataka wananchi wajiandae kuunganisha umeme kwenye nyumba zao za makazi na biashara.

“Rais wetu Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme na amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa licha ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa, pia wananchi hatolazimika kulipia gharama za nguzo pamoja na gharama za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari zimeshalipiwa na Serikali.

Vilevile, Waziri Mkuu alisema Serikali imeboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya na kwamba haitaki kuona mwananchi anakwenda maeneo hayo na kukosa huduma.

“Magufuli alipoingia madarakani aliongeza bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 31 na kufikia sh. bilioni 269, hatutarajii kusikia mgonjwa amekwenda zahanati akaandikiwa cheti na kisha akaelekezwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi,”amesema.

Waziri Mkuu amesema ni lazima dawa zipatikane katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya kulingana na hadhi ya eneo husika kama zahanati lazima dawa zinazotakiwa kuwepo kwenye zahanati ziwepo, kadhalika kituo cha afya na hospitali.