October 20, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Changamoto walizokumbana nazo watoto mlipuko wa kwanza wa Uviko 19 zatajwa

Na Judith Ferdinand,TimesMajira,Online Mwanza

WATOTO wanaioshi na kufanya kazi mtaani Wilaya ya Ilemela na Nyamagana kipindi cha mlipuko wa kwanza wa COVID-19,ulipoingia nchini hapa walikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo jamii

KUNYANYAPALIWA ni miongoni mwa changamoto walizokutana nazo watoto wanaioshi na kufanya kazi mtaani Wilaya ya Ilemela na Nyamagana wakati wa mlipuko wa kwanza wa Uviko 19 Machi, mwaka jana.

Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa Shirika linalojishughulisha na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani la Railway Children Africa (RCA) Mkoa wa Mwanza, Irene Wampembe,wakati akizungumza na majira ofisini kwake jijini Mwanza.

Wampembe, amesema shirika hilo linahudumia watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana, ambapo baada ya corona kuingia nchini Machi mwaka 2020,shirika hilo lilipata changamoto kadhaa hasa watoto na vijana wanaowahudumia,ikiwemo jamii kuwanyanyapaa.

Amesema jamii iliwanyanyapa watoto wa mtaani kipindi cha mlipuko wa kwanza wa Covid-19, kwani ilikua inaona watoto hao wanaweza kuwaletea zaidi corona kutokana na mazingira wanayoishi na mahali wanapo lala.

Amesema,kipindi hicho Serikali iliweza kuhamasisha sana masuala ya kunawa mikono,kutumia vitakasa mikono,kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja.

“Watu walikuwa wanawafukuza watoto hao, mfano wenye maduka na hoteli walikuwa hawawaruhusu watoto hao kusogelea sehemu zao za biashara kwa ajili ya kunawa kama vile ilivyoelekezwa,”amesema.

“Walikuwa wanawafukuza kwa sababu walikuwa wanawaona ni wachafu,hivyo walikuwa hawatakiwi kunawa na kutumia vifaa vyao lakini pia kuzunguka kwao mtaani kulionekana kama tishio la kuweza kusababisha mlipuko zaidi,pia hawana uwezo wa kupata huduma za kunawa na kupata vifaa vya kujikinga na corona hivyo walikuwa wanafukuzwa na watu mitaani,”amesema Wampembe.

Pia amesema,changamoto nyingine ni mapokeo ya ugonjwa huo ilionekana kuwa kuna ule mtazamo kuwa watu weusi hawapati Covid-19,kwa hiyo hata watoto wa mtaani walichukulia kwamba hawawezi kupata ugonjwa huo kwani waliamini siyo wa watu wenye shida na maskini kama wao,bali ni wa watu matajiri.

“Hivyo ilikuwa changamoto hata kwa sisi shirika,hata tulipokuwa tukiwapatia elimu ya kina,walikuwa hawaitilii sana maanani kwa sababu walikuwa hawaamini kwanza kama Covid-19 ipo na walikuwa hawaamini kama corona inaweza kuwapata,”amesema.

Meneja Mradi wa Shirika la Railway Children Africa, Irene Wampembe, akizungumza na TimesMajira,Online ofisini kwake juu ya changamoto walizopata watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kipindi cha mlipuko wa kwanza wa COVID-19 nchini hapa. Picha na Judith Ferdinand

Sanjari na hayo amesema,hatua walizochukua baada ya kutambua watoto hao wa mtaani wanapata changamoto ya kupata huduma za kunawa mikono,kupitia mradi walijenga mabomba ya kunawa mikono hasa maeneo ambayo watoto wanapatikana zaidi.

“Kwa kushirikiana na idara ya maji tulijenga sehemu ya kunawia mikono watoto hao eneo la Kamanga Ferry,kwenye kituo chetu cha watoto ambacho tunakutana nao watoto cha smart school pamoja na stendi ya Nyegezi,ambako ndipo watoto wanapatikana ili wanapohitaji huduma hiyo ya kunawa mikono na kunywa wanapata,”amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Familia wa Shirika hilo Adam Mashimba,amesema changamoto nyingine ni hofu kutanda kwa watoto kutokana na hali ilivyokuwa,kwamba ni tatizo linalotokana na mfumo wa upumuaji na ukizingatia wao mazingira wanayoishi na watu hawakutaka kabisa kuwasogelea hali iliowaongezea hofu ya kuwa inaweza kusababisha wakapoteza maisha.

Naye Mkuu wa Idara ya Vijana na Watoto wa shirika hilo,Ayoub Hezron amesema hatua walizochukua za kuwakinga na janga la corona licha ya kuwapima joto na kutambua kiwango cha joto, walihakikisha kabla ya kuanza kufanya kazi nao waliwaanda kwa kuwapatia barakoa, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono ili wawe salama wasipatwe na maambukizi.