June 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zambia yapongeza mafanikio ya Tanzania Sekta ya Umeme

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati nchini Zambia, Arnold Simwaba, amesema kuwa Tanzania na Zambia zimeendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa TAZA (Tanzania–Zambia Power Interconnection Project), wenye lengo la kuunganisha gridi za umeme za nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote.

Simwaba ameyasema hayo Juni 25, 2026, mkoani Dodoma, wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha wajumbe kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya Nishati ya Zambia, Mamlaka ya Umeme Vijijini ya Zambia pamoja na Shirika la Umeme Zambia (ZESCO), kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuboresha huduma za umeme.

Ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya umeme baada ya miradi mingi ya umeme kukamilika nchini. Aidha, amesifu jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi hususani matumizi ya umeme katika shughuli za kupikia.

Simwaba amesema ushirikiano kati ya Zambia na Tanzania katika sekta ya nishati utasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme na kuharakisha matumizi ya nishati safi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Mkutano huu ni muhimu kwetu kwa sababu tumekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu. Tanzania inafanya kazi kubwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme, lakini pia katika utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa upande wetu, mbinu tunazotumia Zambia katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi zina tofauti kidogo. Ndiyo maana tumekuja kujifunza kutokana na mafanikio yenu,” amesema Simwaba.

Kwa upande wake, Meneja wa Miradi ya Usambazaji Umeme wa TANESCO, Christopher Mbwija, amesema Tanzania na Zambia zinaendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme kati ya Tanzania na Zambia (TAZA), ambao ukikamilika utakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha biashara ya umeme kikanda.

Amesema mradi huo utaimarisha uhusiano wa mifumo ya umeme kati ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kanda ya Kusini mwa Afrika kupitia jumuiya za East African Power Pool (EAPP) na Southern African Power Pool (SAPP), hivyo kuongeza fursa za biashara ya umeme na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda huo.

Ugeni huo kutoka Wizara ya Nishati ya Zambia, Mamlaka ya Umeme Vijijini ya Zambia na Shirika la Umeme Zambia (ZESCO) ulifanya ziara rasmi nchini kuanzia Juni 21, 2026, ambapo ulitembelea taasisi mbalimbali za sekta ya nishati nchini Tanzania, zikiwemo Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na TANESCO.