June 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya elimu kunufaika na Mil. 847

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbeya imepokea zaidi ya Sh. Mil. 847 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa kike na wa kiume kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule za msingi na sekondari.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Beatrice Ngutu amesema fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya elimu huku mafunzo yakitolewa kwa kamati za ujenzi wa shule zilizonufaika ili kuimarisha usimamizi na matumizi sahihi ya fedha.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yanategemea weledi uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wanaosimamia rasilimali za umma huku akieleza kuwa baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni ucheleweshaji wa miradi unaochangia ongezeko la gharama ukiukwaji wa taratibu za manunuzi ya umma na ujenzi usiozingatia viwango vya kitaalamu.

Amesema washiriki wa mafunzo wanapaswa kutumia maarifa watakayopata kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kwa ufanisi na uwazi pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia sheria kanuni na miongozo iliyopo.

Amesema hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhujumu fedha za miradi ya maendeleo huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

Amesema washiriki wanapaswa kuwa mabalozi wa usimamizi bora wa miradi katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati kwa ubora unaotakiwa na kuwanufaisha wananchi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza uwezo wa kusimamia majukumu yao ya kila siku na kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika shule.

Mmoja wa washiriki Abishai Aron pamoja na mjumbe wa kamati ya ujenzi wa Shule ya sekondari Ikhoho Oseba Mbilinyi wamesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yataongeza uelewa wa usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za maendeleo.