August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nungu:Haki za wabunifu zilindwe


TUMEB ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki za wabunifu nchini, ikisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha bunifu zinaleta tija kwa wabunifu wenyewe na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.


Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema hayo baada ya kutembelea Banda la Vijana linalowashirikisha vijana wanaoshiriki Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samweli Malecela, Nzuguni, Dodoma.


Alisema Serikali kupitia COSTECH inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kwa kuwaunganisha na taasisi mbalimbali, kuwawezesha kupata mitaji na kuwasaidia kulinda haki zao za ubunifu ili bunifu zao ziweze kufikia hatua ya kibiashara.


Kwa mujibu wa Dkt. Nungu, COSTECH imeweka mifumo mbalimbali ya kusaidia wabunifu, ikiwemo utoaji wa fedha za kukuza bunifu (seed funding), dhamana za mikopo (guarantee schemes) pamoja na kuwaunganisha wabunifu na taasisi zinazoweza kuwasaidia kupata mitaji.


Alisema hata hivyo, vijana bado wanakabiliwa na changamoto zinazoweza kuchelewesha safari ya bunifu zao kutoka hatua ya ubunifu hadi sokoni, zikiwemo usajili wa kampuni, utambulisho wa bidhaa na upatikanaji wa vibali mbalimbali.


“Tumebaini bado kuna changamoto zinazowakabili vijana hawa, ikiwemo usajili wa kampuni, utambulisho wa bidhaa zao na upatikanaji wa vibali mbalimbali. Ndiyo maana tumekutana nao pamoja na wadau wengine ili kusikiliza changamoto hizo na kutafuta suluhisho la pamoja,” alisema.


Dkt. Nungu alisema COSTECH ilipata fursa ya kukutana na wabunifu waliopo ndani na nje ya Programu ya BBT wakati wa ziara hiyo, ambapo alisikiliza changamoto na maoni yao kuhusu mazingira ya ubunifu nchini.


Alisema kikao hicho pia kilihusisha wadau mbalimbali, wakiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Wakala wa Mbolea na taasisi nyingine zinazohusika na sekta ya kilimo na ubunifu.


Alieleza kuwa maoni yaliyotolewa na vijana yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau husika, kwa lengo la kuboresha mazingira ya ubunifu na ujasiriamali nchini.


Dkt. Nungu alitolea mfano wa kijana aliyebuni teknolojia ya kutengeneza mbolea kwa kutumia nywele, akisema baada ya kuanza ubunifu huo bila msaada wa COSTECH, baadaye alipata msaada wa Tume katika usajili na ulinzi wa haki zake za ubunifu.


Alisema hatua hiyo ilimsaidia kijana huyo kupata uwekezaji na fedha kutoka nje ya nchi, jambo alilolitaja kuwa ushahidi wa umuhimu wa kulinda haki miliki za wabunifu.


“Hii inaonyesha kuwa msaada wa Serikali si fedha pekee, bali pia ni kujenga mazingira rafiki yanayowezesha wabunifu kulinda kazi zao, kuziboresha na kuzifikisha sokoni,” alisema.


Katika hatua nyingine, Dk. Nungu alisema vijana hao wameiomba Serikali kupitia COSTECH kufikisha ujumbe kuhusu utaratibu wa marejesho ya mikopo inayotolewa na halmashauri.


Alisema vijana wameeleza kuwa muda wa kuanza kurejesha mikopo hiyo ni mfupi na hauwapi nafasi ya kutosha kuendeleza miradi yao kabla ya kuanza kufanya marejesho.


Kwa mujibu wa Dk. Nungu, COSTECH imepokea ombi hilo na italijadili kwa kushirikiana na mamlaka husika ili kutafuta namna ya kuboresha mazingira ya mikopo kwa wabunifu na wajasiriamali vijana.


Alisema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kushirikiana na vijana katika kuimarisha mfumo wa ubunifu, utafiti na teknolojia, huku lengo likiwa ni kuhakikisha bunifu zinazozalishwa nchini zinapata mazingira yanayowezesha kukua na kufikia soko.