Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
MFUGAJI wa panya kutoka Kata ya Kitwiru, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Evaristo Mgina, amekuwa kivutio katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, baada ya kuonesha panya wanaofugwa kwa urafiki na binadamu na kutumika kwa matumizi mbalimbali.
Akizungumza na Timesmajira Agosti 7, 2026, Mgina amesema alianza ufugaji huo baada ya kupata panya hao kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), na tangu wakati huo ameendelea kuwazalisha hadi kugeuza ufugaji huo kuwa fursa ya biashara.

Amesema panya hao wana matumizi mbalimbali, ikiwemo kufugwa kama wanyama wa mapambo majumbani, kutumika kama chakula cha mbwa na paka, pamoja na kusaidia mafunzo ya vitendo katika masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
“Panya hawa pia wanaweza kusaidia katika kudhibiti panya waharibifu wa majumbani, kwa kuwa harufu na tabia zao huwafanya panya hao kuwaogopa na kuondoka katika maeneo wanayoishi,” amesema Mgina.
Ameongeza kuwa panya hao ni rafiki kwa binadamu na ni rahisi kuwafuga, huku akieleza kuwa katika baadhi ya nchi hutumika pia katika shughuli maalumu za kutambua mabomu ya ardhini.
Kwa mujibu wa Mgina, jozi ya panya jike na dume kwa ajili ya kuzalisha huuzwa kwa Sh200,000, huku dume mmoja anayelenga kufukuza panya waharibifu akiuzwa kwa Sh50,000.
Amesema kwa shule zinazohitaji panya hao kwa ajili ya mafunzo ya sayansi, panya mmoja huuzwa kwa Sh20,000.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema serikali inamtambua mjasiriamali huyo na imekuwa ikishirikiana naye, ikiwemo baadhi ya shule ndani ya halmashauri kununua panya hao kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi.
Mlawa amesema halmashauri itaendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kukuza biashara zao.
Mkurugenzi huyo amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi.

More Stories
EWURA yaonya wanaofanya biashara bila leseni
UDOM yajidhatiti katika bunifu kutatua changamoto za jamii
Wakulima wapewa mbinu kukabiliana na Sumukuvu