August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaweka mkazo kuongeza thamani mazao kupitia viwanda

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline

SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanaongezewa thamani kupitia viwanda, hatua inayolenga kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Kilimo

Mkutano huo ulilenga kujadili namna maarifa, mafanikio na changamoto katika sekta mbalimbali zinavyoweza kutumika kama fursa za kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa.

Londo amesema wakulima, wafugaji na wavuvi wanapaswa kutumia maarifa na teknolojia za kisasa katika uzalishaji ili kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha ubora wa bidhaa na kuzifikisha katika masoko ya ndani na kimataifa.

“Matumizi ya taarifa sahihi na maarifa ndiyo msingi wa kuongeza tija na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara kupitia TARURA, kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, pamoja na kuendelea kutoa ruzuku ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa Utaratibu wa Koroba nchini, Geoffrey Kilenga, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki, SADC pamoja na nchi za Ulaya, Asia na Marekani.

Hata hivyo, amesema mafanikio katika masoko hayo yanategemea uzalishaji wa mazao yenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Kilenga amesema mkutano huo umeonesha umuhimu wa kutumia sayansi na teknolojia katika kuthibitisha ubora wa mazao, akieleza kuwa teknolojia hiyo itawarahisishia wakulima, wasindikaji na wanunuzi kutambua ubora wa mazao kabla ya kuyapeleka sokoni.

Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda afya za walaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Aidha, Kilenga amewataka wananchi kununua mazao kutoka maeneo yanayozingatia viwango vya ubora na kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha usalama wa chakula na afya ya jamii.