Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Chunya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imeanza utaratibu wa kuwapeleka mahakamani baadhi ya wanachama wa vikundi vilivyokopa mikopo ya asilimia 10 na kushindwa kurejesha, huku deni linalodaiwa kufikia sh.milioni 600.
Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi, lakini baadhi yao wameshindwa kurejesha fedha hizo kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 6,2026 kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo, ikiwemo mpango wa mikopo ya asilimia 10, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona amesema, urejeshaji wa mikopo hiyo umekuwa changamoto.
Kambona amesema,halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja, lakini baadhi ya vikundi vimeshindwa kurejesha fedha kwa wakati, hali iliyosababisha kuanza kwa taratibu za kisheria.
“Marejesho yake yamekuwa hafifu kwa vikundi hivi mpaka tumefikia hatua ya kuanza taratibu za kuwapeleka mahakamani ili fedha hizi ziweze kulipwa,” amesema.
Pia amesema,halmashauri itaendelea kutoa mikopo hiyo, na kwa mwaka huu inatarajia kutoa zaidi ya sh.bilioni moja, huku akisisitiza kuwa urejeshaji wa mikopo ndiyo changamoto kubwa inayohitaji ushirikiano wa Maofisa Maendeleo ya Jamii na wananchi.
Hata hivyo amesema,baadhi ya kata zimewekewa utaratibu wa kutonufaika na mikopo mipya hadi zitakapomaliza madeni ya mikopo ya awali.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chunya, Esther Kondobole amesema,jumla ya sh. milioni 600 zinadaiwa kutoka katika vikundi vya kata mbalimbali, ikiwemo Chokaa, Itewe, Sangambi na Makongolosi.
Kondobole amesema,halmashauri inaendelea kuvifuatilia vikundi hivyo na kuchukua hatua zinazohitajika, ikiwemo kuandaa utaratibu wa kuvifikisha mahakamani ili kurejesha fedha hizo.
Amesema changamoto ya urejeshaji imeonekana kwa baadhi ya makundi ya wanufaika, huku akitaja vijana wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini kuwa miongoni mwa wanaokabiliwa na changamoto za ufuatiliaji kutokana na kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine,leo anaweza kuwa katika kata hii, kesho akasikia kuna dhahabu eneo lingine na kuondoka, hivyo anapotafutwa inakuwa vigumu kumpata.
Aidha, Kondobole amesema,shughuli za uchimbaji madini zina changamoto zake katika urejeshaji wa mikopo kwa sababu wanufaika huingia mikataba na halmashauri ya kurejesha fedha baada ya kipindi maalumu, lakini upatikanaji wa mapato kutokana na uchimbaji hauwezi kutabirika.

More Stories
Ilemela yakusanya bil. 4.37
UN:Mabunge yana nafasi kubwa kuharakisha Maendeleo
Mwenge wataka daraja Ileje kukamilika kwa wakati