Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27 imekusanya kiasi cha sh.bilioni 4.37 kati ya sh.bilioni 19.25 iliyopanga kukusanya katika mwaka huo wa fedha sawa na asilimia 23 ya lengo, hadi kufikia Septemba 30, 2026.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Wakili Goodluck Lukandiza akisoma taarifa Oktoba 7,2026 kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ummy Wayayu, katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekekalezaji robo ya kwanza Julai-Septemba,2026,ambapo amesema,katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, halmashauri hiyo ilielekeza kiasi cha sh.bilioni 4.48 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika kipindi hicho halmashauri hiyo imepeleka kiasi cha sh.bilioni 4.48,fedha kutoka mapato ya ndani,Serikali Kuu na Wahisani ambapo kiasi cha sh.bilioni.3.23 ni fedha za bakaa( fedha zilizobaki kutoka mwaka wa fedha 2025/2026) na sh.bilioni 1.25 fedha za robo ya kwanza mwaka wa fedha 2026/2027 zilizotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kata za halmashauri hiyo.
Amesema,fedha zilizobaki kutoka mwaka uliopita zilitumika katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ya sekondari sh.milioni 156.78 milioni, elimu ya msingi sh.milioni 873.59, utawala sh.milioni 837.27,afya sh.milioni 267.77, miundombinu sh.milioni 51.83, kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika sh.milioni 144.70 pamoja na viwanda, biashara na uwekezaji sh.miliomni 900.
Pia amesema,katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia mapato ya ndani ya robo ya kwanza, kiasi cha sh.milioni 177 zilitengwa kwa elimu ya sekondari, sh.milioni 146.8 elimu ya msingi,sh.milioni 370 afya,sh.milioni 221.22 maendeleo ya jamii,sh.miliono 234.30 miundombinu,sh.milioni 47.3 viwanda, biashara na uwekezaji,sh.milioni 50 kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika huku sh.milioni 8.8 mipango na uratibu.
Hata hivyo amesema,katika matukio ya robo hiyo, Halmshauri ya Manispaa ya Ilemela ilishika nafasi ya kwanza katika kundi la Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye maonesho ya Nanenane ya mwaka 2026, ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo mwaka 2025.
Pia, Agosti 18, 2026, ilipokea vifaa vya maabara na vitabu vya sayansi kutoka Serikali Kuu kupitia TAMISEMI kwa ajili ya Shule za Sekondari Kisenga na Mwaselundi zilizojengwa kupitia mradi wa SEQUIP.Lengo la vifaa na vitabu hivyo ni kuongeza ufanisi wa ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa vitendo shuleni.
Diwani wa Kata ya Buzuruga Manusura Sadick amesema,katika robo ya kwanza wamefanikiwa kukusanya asilimia 23 ya mapato ya ndani ingawa walipaswa kukusanya asilimia 25,hivyo bado wanahitaji kuongeza kasi ili kufikia lengo la asilimia 100.
“Najua tunakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo changamoto za mfumo,lakini ni muhimu kuongeza juhudi na usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo tuliyoainisha katika bajeti zetu,”amesema Sadick na kuongeza:
“Pamoja na changamoto hizo, naomba tumpongeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na menejimenti yake kwa kazi wanayoifanya. Kukusanya mapato siyo kazi rahisi, hasa katika kipindi ambacho tunatumia mfumo mpya,muhimu kuendelea kuwaunga mkono na kuwahamasisha ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya maendeleo ya kata zetu,”.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kitangiri Donald Ndaro amesema, katika taasisi zao za elimu msingi na sekondari wapo walimu wanaojitolea, ‘volunteers’,hivyo alishauri watambuliwe rasmi angalau katika kuwezeshwa posho.
“Walimu hawa wamekuwa wakijitolea kusaidia walimu wetu wa shule za msingi na sekondari kwa juhudi kubwa. Na changamoto ni upataji wa , ajira,kwani Serikali inapotangaza ajira wanakosa wanaingia wapya kabisa, ambao hata hawajajitolea,” amesema Ndaro.


More Stories
Chunya kuwaburuta mahakamani wadaiwa wa mil.600
UN:Mabunge yana nafasi kubwa kuharakisha MaendeleoÂ
Mwenge wataka daraja Ileje kukamilika kwa wakati