August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yasihi matumizi salama ya umeme na LPG


Na Joyce Kasiki, Dodoma


MAMLAKA  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahimiza wananchi kuzingatia taratibu za usalama wanapotumia umeme na gesi ya mafuta ya petroli (LPG), ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia ajali zinazoweza kuhatarisha maisha pamoja na kusababisha uharibifu wa mali.

Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa EWURA Kanda ya Kati, Hawa Lweno, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dk. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Lweno alisema bado kuna wananchi wanaotumia mifumo ya umeme na gesi bila kuzingatia kanuni za usalama kutokana na uelewa mdogo kuhusu matumizi sahihi ya huduma hizo.

Alifafanua kuwa kazi za ufungaji wa nyaya za umeme zinapaswa kufanywa na mafundi wenye taaluma na wanaotambulika rasmi ili kuzuia hitilafu zinazoweza kusababisha moto, mshtuko wa umeme na madhara mengine.

Kwa upande wa matumizi ya gesi ya LPG, aliwataka watumiaji kuhakikisha mitungi pamoja na vifaa vinavyohusika vinakidhi viwango vya usalama na vinakaguliwa mara kwa mara, huku wakifuata maelekezo ya matumizi yaliyotolewa na watengenezaji.

Alisema EWURA inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane na mikutano mbalimbali ya wananchi kama fursa ya kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya nishati na umuhimu wa kutumia vifaa vinavyokidhi viwango vilivyowekwa.

Aidha, aliwataka wananchi kutoweka rehani usalama wao kwa kufanya matengenezo ya mifumo ya umeme au gesi bila ushauri wa wataalamu, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza hatari ya ajali.

Lweno alisema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama na yenye tija ya nishati nchini