Na Mwandishi Wetu, Dodoma
UBUNIFU wa kutengeneza mafuta ya asili yanayotokana na mbegu za zabibu uliofanywa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Omari Kongolo, umekuwa kivutio katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, huku ukilenga kuongeza thamani ya zao hilo na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za ngozi.
Kongolo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Kozi ya Sayansi ya Uhandisi wa Kemia na Uchakataji, amesema ubunifu huo umetokana na maarifa aliyoyapata chuoni kupitia kozi anayoisomea.

Akizugumza katika maonesho hayo amesema mafuta hayo ni ya asili na hutumika kwa ajili ya ngozi na uso, yakisaidia kuboresha afya ya ngozi kwa watu wenye changamoto mbalimbali.
“Nilianza kutengeneza mafuta haya miaka miwili iliyopita na tangu wakati huo yamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wanaoyatumia,” amesema Kongolo.
Ameeleza kuwa mafuta hayo husaidia kuipa ngozi unyevunyevu na mng’ao wa asili, kutibu ngozi zilizoharibika kutokana na matumizi ya mafuta makali pamoja na kulinda ngozi dhidi ya miale ya jua.
Kwa upande wa nywele, amesema bidhaa hiyo husaidia kukuza na kujaza nywele, kuondoa mba na muwasho, kuzipa nywele mng’ao na kuzuia nywele kukatika.
Kongolo amesema mwitikio anaoupata kutoka kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo unaonyesha kuwa Watanzania wanaendelea kuthamini bidhaa za ubunifu wa ndani zinazotokana na malighafi za asili.

Ameongeza kuwa anaendelea kuboresha bidhaa hiyo ili iweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi, kuchangia maendeleo ya sekta ya ubunifu na kuongeza thamani ya mazao ya zabibu nchini.
Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda lao katika Maonesho ya Nanenane ili kujionea bunifu mbalimbali zinazotokana na mazao ya asili.

More Stories
T-CAMS yaleta mapinduzi sekta ya uwakala wa forodha
Nanauka apongeza Kariakoo Kwa kuwezesha vijana Kibiashara
Uzalishaji mbegu bora waongezeka kwa asilimia 55 nchini