August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nanauka apongeza Kariakoo Kwa kuwezesha vijana Kibiashara

Na Mwandishi wetu Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amepongeza Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa kuwapatia vijana maeneo ya biashara, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Akizungumza baada ya kutembelea banda la Shirika la Masoko ya Kariakoo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo yanayofanyika katika Viwanja vya John Samwel Malecela, Nzuguni mkoani Dodoma, Nanauka alisema utoaji wa fursa za biashara kwa vijana unawajengea uwajibikaji na kuwapa nafasi ya kujiongezea kipato.


Waziri Nanauka aliwataka vijana kuendelea kutumia fursa mbalimbali zinazowekwa na Serikali, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira wezeshi ili kuwawezesha vijana kukuza biashara zao na kunufaika na uwekezaji unaofanyika nchini.


Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashraph Abdulkarim, alisema shirika limetenga maeneo ya biashara kwa vijana katika masoko ya Kariakoo na Tabata kwa lengo la kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.


Alisema vijana ndio kundi kubwa la wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo, wakijihusisha na biashara mbalimbali zikiwemo nguo, bidhaa za majumbani, pembejeo za kilimo, pamoja na biashara za matunda, mboga, nyanya, viazi na dagaa.


CPA Abdulkarim aliongeza kuwa masoko hayo yamezalisha ajira nyingi kwa vijana, ambapo wamiliki wa maeneo ya biashara pamoja na wazabuni wa huduma za usafi na ulinzi wameendelea kutoa kipaumbele kwa ajira za vijana.