April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ummy afunguka miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia

Na Penina Malundo,TimesmajiraOnline,Dar

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya afya imeendelea kuwa imara na kusonga mbele katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu kutoka vituo vya afya 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024.

Waziri Ummy ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka mitatu ya Rais Samia katika Mageuzi makubwa katika sekta ya Afya.

Amesema kwa upande wa miundombinu, Serikali imeweza kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano.

Amesema maboresho hayo yamegharimu kiasi cha jumla ya sh. Trilioni 1.02 na yalifanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiendeleza ujenzi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa mipya mitano ambayo ni Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita.

Ummy amesema licha ya hospitali hizo kuendelea na ujenzi pia tayari zimeanza kutoa huduma kwa wananchi kwa maeneo husika na kuweza kupata matibabu.

“Ongezeko la vituo vya kutoa huduma za afya nchini na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika yametuwezesha kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi kama tunavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025,”amesema na kuongeza;

“Hivi sasa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilometa tano ya maeneo yao wanayoishi lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030.”

Amesema katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa wagonjwa, Serikali ya Rais Samia imenunua vifaa Tiba vya Uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya sh. bilioni 290.9 ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa hadi Hospitali za Rufaa za Mikoa (RRHs) na Halmashauri.

Ummy amesema miongoni mwa idadi ya vifaa vilivyonunuliwa na Serikali ya awamu ya sita ni pamoja na MRI,CT SCAN,MINI ANGIO SUIT ,DIGITAL X-RAY,ULTRASAOUND, CT SCAN,FLUOROSCOPY, DIGITAL X-RAY,ULTRASOUND,ECHOCARDIOGRAM PET SCAN na CATHLAB.

Alisema katika huduma za kipimo cha CT Scan,kwa sasa zinapatikana katika Hospitali takribani 27 kati ya Hospitalii 28 za rufaa za Mikoa nchini.

Ummy amesema kwa mwaka 2023, jumla ya wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo cha CT Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo huduma hizo zilikuwa hazitolewi katika hospitali za Rufaa za Mikoa hapo awali.

Ummy alisema pia katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia wameweza kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kwa asilimia 80 na kuimarisha kwa huduma za uzazi, mama na mtoto.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yamepelekea kupunguza vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa sasa .

“Vifo vya watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022,”‘amesema.

“Vifo vya watoto umri chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 33 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi sasa, huku vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa chini ya siku 28) vimepungua kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 24 kwa vizazi hai 1,000 hadi sasa,”amesisitiza.

Aidha amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt Samia katika kuimarisha huduma ubingwa na ubingwa bobezi umewezesha wananchi wengi kupata huduma hizo ndani ya nchi kwa gharama nafuu badala ya kuzitafuta nje ya nchi.

Ummy alisema uwekezaji huo umeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi na hivyo kuifanya Tanzania kuwa Kituo cha Tiba Utalii kwa ukanda wa nchi za afrika mashariki na kusini mwa afrika.

Amesema kumekuwa na ongezeko la raia wa kigeni kuja Tanzania kwa ajili ya matibabu ambapo kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wa Tiba Utalii waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa 3,957 mwaka 2022 na wagonjwa 75 mwaka 2021.