April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia amwaga trilioni 6.720/- kuboresha sekta ya afya

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

MIAKA mitatu ya RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Sh. trilioni 6.720 kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya afya kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuimarisha na upatikanaji wa dawa na ununuzi wa vifaa tiba.

Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa ya mafanikio na mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini katika kipindi cha miaka mitatu, chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, cha uongozi wa Rais Samia umefanyika uwekezaji katika miundombinu ya kutolea huduma za afya, ambapo vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024.

“Hii ni sawa na ongezeko la vituo 1,061, kwa sasa asilimia 80 ya watanzania wanapata huduma za afya ndani ya km 5 ,”alisema Waziri Ummy.

Alisema serikali imetumia sh trilioni 1.02 kwa ajili ya kujenga na kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwemo ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika Mikoa mipya mitano ikiwemo kukamilisha kwa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.

Pia kukamilisha ujenzi wa Hospitali mpya za Rufaa za Mikoa mitano ambayo ni Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita pamoja na kuhamisha hospitali tano kutoka majengo yake ya zamani kwa kujenga Hospitali mpya katika maeneo mapya ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, Shinyanga, Singida, Mara na Lindi.

Aliongeza kuwa serikali imekarabati na kujenga majengo mapya ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Ligula (Mtwara), Sekoutoure (Mwanza), Maweni(Kigoma), Sumbawanga(Rukwa) na Kitete(Tabora).

Alisema kuongezeka kwa vituo vya kutoa huduma za afya nchini na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika yamewezesha kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa wagonjwa, serikali ya Rais Samia imetoa sh bilioni 290.9 kununua vifaa tiba vya uchaguzi na matibabu ya wagonjwa vinavyopatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya taifa hadi hospitali za Rufaa za Mikoa (RRHs) na Halmashauri.

Alisema hadi mwaka 2021 katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, kulikua na mashine ya MRI 7 ambapo katika kipindi cha miaka mitatu (Machi 2024) zilinunuliwa mashine mpya 6 na kufanya jumla yam shine hizo kuwa 13 nchi nzima.

Alisema mwaka 2021 kulikuwa na mashine za CT Scan 13 ambapo hadi Machi 2024 mashine mpya 32 zilinunuliwa na kufanya jumla ya mashine kufikia 45 nchi nzima lakini pia hadi mwaka 2021 kulikuwa na mashine za Digital X Ray zilikuwa 147 ambapo katika kipindi cha miaka mitatu zimeongezeka mashine 199 na kufanya jumla yam ashine hizo kuwa 346.

Waziri Ummy alisema mwaka 2021 kulikuwa na mashine za Utrasound 476 ambapo katika kipindi cha miaka mitatu serikali ilinunua mashine 192 na kufanya jumla yam ashine kufikia 668 nchi nzima.

Alisema huduma za CT Scan sasa zinapatikana katika Hospitali 27 kati ya Hospitali 28 za Rufaa za Mikoa nchini lakini pia vitanda vya kulaza wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini vimeongezeka kutoka 86,131 mwaka 2021 hadi vitanda 126,209 Machi 2024.

Amefafanua ongezeko hilo limesaidia kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za afya hususan huduma za afya ya mama na mtoto.