April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikwete aanika mbinu za kutokomeza ugonjwa wa malaria

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete amelishauri Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania (NMCP) kutumia mbinu ambazo mataifa mengine imezitumia na kufanikiwa kutokomeza ugonjwa huo kwenye nchi zao.

Kikwete alitaja nchi hizo tatu za Afrika ambazo ambazo zimefanikisha kutokomeza ugonjwa huo kuwa ni Mauritius, Algeria na Cape verde. Alisema nchi hizo zimepata mafanikio hayo kwa kutumia mbinu nne.

Kwa mujibu wa Kikwete, mbinu hizo ni pamoja na matumizi ya dawa za malaria, vyandarua vilivyotiwa dawa, upuliziaji wa dawa kwenye makazi na kuua mazalia ya mbu

Kikwete ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Kutokomeza Malaria Duniani GMP, aliyasema hayo jana katika kikao cha tatu cha Baraza la kutokomeza Malaria nchini.

Kwa mujibu wa Kikwete, inawezekana kutokomeza ugonjwa huo, endapo watawatumia wadau mbalimbali kwani Serikali pekee haitaweza. “Hali si nzuri inatubidi kuongeza kasi na nguvu kwa ajili ya kutokomeza Malaria.

Kikwete alisema ni muhimu kuongeza jitihada za kutokomeza ugonjwa wa malaria kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 11 duniani zinazoongoza kwa maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Kwa pamoja nchi hizo zimeweka rekodi ya maambukizi ya milioni 167 sawa na asilimia 67 ya maambukizi yote duniani. Pia nchi hizo zimechangia asilimia 73 ya vifo huku asilimia 78 imechangiwa na vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo, Leodegar Tenga amesema wanaendelea kuchukua hatua kukamilisha malengo yake ili kutokomeza malaria nchini kufikia mwaka 2030 kwa kuongea na makundi mbalimbali yenye ushawishi.

“Kwanza tumeanza mazungumzo na viongozi wa dini na wamekubali kutoa elimu kwa waumini wao ili iwe rahisi kutokomeza ugonjwa huo,”alisema .

Aliongeza kuwa wameanza mazungumzo na tasnia ya michezo kutokana na wingi wao ili kuone namna watakavyotusaidia kufikisha ujumbe kwa upande huo.

Mkuu wa Programu Wizara ya Afya, Dk Catherine Joachim, amesema wataendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha kampeni zote za kutokomeza malaria zinafanikiwa.

“Tupo tayari kufanya yote ambayo tumeshauriwa na tutahakikisha tunafanyia kazi ushauri,”alisema.

Takwimu za Wizara ya Afya za mwaka huu zinaonesha watu milioni 19.8 walipimwa ugonjwa wa malaria kati yao watu milioni 3.46 walikutwa na ugonjwa huo.