April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mhagama: OSHA wamesamehe toza 11

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online,Dar

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana,Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema tozo ambazo Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) wamezisamehe zimefika tozo 11.

Aidha, amesema ukichukua tozo zote ambazo OSHA wameziondoa zina thamani ya fedha ya sh. bilioni 50 kwa hiyo kwa sasa fedha hizo zimebaki huko huko kwa wafanyabiashara na wawekezaji, wanachotakiwa ni kuimarisha miundombinu na pia kununua vifaa vya wafanyakazi.

Mhagama amesema hayo jana, jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Banda ya OSHA katika Maonesha ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya matokeo ya siku 100 za utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tunachojivunia hapa OSHA ni maagizo ya Rais Samia yalikuwa wazi kabisa kwamba ziko tozo ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara, lakini hata kwa wawekezaji, mwaka uliopita kwenye bajeti tulipunguza tozo saba,” amesema Mhagama na kuongeza;

“Lakini jambo ambalo nataka niwapongeze OSHA kwa mwaka huu wa fedha, kwanza wameridhia zile tozo saba ziendelee kubakia vile vile, ambavyo zimepunguzwa na hazikurudishwa tena, lakini pia wamepunguza tozo zingine nne.”

Amesema tozo saba zilizopunguzwa muhula uliopita bado zinaendelea, lakini pia mwaka huu wameongeza tozo zingine nne zenye kero kufanya tozo zote zilizoondolewa kufikia 11.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana,Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akisani kitabu cha wageni alipotembelea Banda Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam jana. Maonesho hayo yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa. Na mpiga picha wetu.

Waziri huyo amesema eneo lingine mahususi ambalo OSHA wamelifanyia kazi kwenye mwaka huu wa fedha na sheria ya fedha imeonesha ni kwamba wanataka kupitia uwekezaji wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini.

Amesema kwa kila anayefungua kituo cha mafuta kuna tozo inayotozwa na OSHA kwa maeneo ya vijijini na sio wa mjini, ambapo kuna tozo kama ya sh. 500,000 ambayo inagawanywa kwa vitu tofauti tofauti.

“OSHA wanapita na kuvikagua vituo walikuwa, ukienda kuwekeza huko lazima ukutane na hiyo tozo kwa hiyo wameipunguza kutoka sh. 500,000 hadi sh. 150,000, tunataka ile ya kuweka petroli na mafuta kwenye vikopo kopo ipungue,

“Na Wizara ya Nishati imeanza kuwa na mfumo na mkakati wa kutengeneza vituo vya mafuta vidogo vidogo kwa ajili ya usalama wa raia, kwa hiyo na sisi tunavyotoa hii tozo unaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na kwa Watanzania wenyewe na hata kama kwa wageni,” amesema

Mhagama amesema, kutakuwa na vituo vidogo vidogo ambavyo ni usalama kwa raia na kuondoa ondoa viashiria vya hatari.