Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
WATU wawili wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kumjeruhi Mihayo Budaga(78), mkazi wa Kitongoji cha Nyambono, kijiji cha Kisamba, Kata ya Lubugu wilayani Magu mkoani humo.
Akizungumza Julai 18,2026 mkoani humo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa,amesema tukio hilo lilitokea Julai 11,2026 majira ya saa 08:00 usiku,ambapo Budaga akiwa amelala nyumbani kwake, ghafla watuhumiwa hao ambao ni Lusana Kaswahili na Mbizo Kaswahili walivamia makazi yake.
Na baada ya hapo watuhumiwa hao walivunja mlango wa kuingilia na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye chumba chake.
Watuhumiwa hao wakiwa ndani, walimshambulia mzee huyo na kumjeruhi kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani upande wa kulia, pamoja na maeneo mbalimbali ya mkono wake wa kulia na kusababisha kuvuja damu nyingi na hali yake kiafya kuwa mbaya.
DCP.Mutafungwa amesema,baada ya jeshi hilo kupokea taarifa hizo, askari walifika haraka eneo la tukio walimchukua majeruhi na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa matibabu lakini kutokana na hali yake kuwa mbaya, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambapo kwa sasa anaendelea vizuri.
Hata hivyo amesema,uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina na kulipiza kisasi kwani watuhumiwa walikuwa wanamtuhumu Mihayo Budaga, kuwa anawaloga ndugu zao.
Aidha amesema,watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa kwa kina na upelelezi ukikamilika, watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake
“Natoa rai kwa wananchi wote wanaoendeleza tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kushambulia watu kwa visingizio vya imani za kishirikina au visasi waache mara moja kwani vitendo hivyo havitafumbiwa macho hata kidogo,”amesema DCP.Mutafungwa.
   Â

More Stories
Watuhumiwa 10 mbaroni kwa utapeli
Upatikanaji wa maji Chunya wafikia asilimia 52
MiXX Yakabidhi Zawadi kwa Washindi wa Kampeni ya Kombe la Dunia