July 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Upatikanaji wa maji Chunya wafikia asilimia 52

Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online- Chunya

MBUNGE wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya, mkoani Mbeya, Masache Kasaka, amesema upatikanaji wa maji jimboni humo,umeongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 52 kwa sasa, tangu alipochaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi.

Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji hususani katika maeneo ya vijijini.Huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi wa Miji 28 ndiyo suluhisho litakalosaidia kumaliza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.

Kasaka ameyasema hayo Julai 18, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Chunya, hasa maeneo ya vijijini ambayo bado yanakabiliwa na uhaba wa huduma hiyo muhimu.

Amesema kukamilika kwa mradi wa Miji 28 kutaiwezesha Serikali kuanza kusambaza maji katika vijiji mbalimbali kisha kufikisha huduma hiyo hadi kwenye vitongoji, hatua ambayo itasaidia kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama.

Pia amesema,Serikali tayari imetenga Dola milioni tano kwa ajili ya uchimbaji wa visima katika maeneo yanayolengwa, huku taratibu zikiendelea za kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chokaa, Joshua Mwambalala, amesema kutokana na umuhimu wa maji katika maisha ya wananchi, wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha changamoto hiyo ya muda mrefu inapatiwa ufumbuzi.

“Kabla ya kuwa Diwani nilihudumu kama Mwenyekiti wa Kitongoji kwa miaka kadhaa, hivyo ninazifahamu changamoto nyingi za wananchi. Nina imani na Mbunge wetu pamoja na Serikali iliyopo madarakani katika kutatua kero hii ya maji,”amesema Mwambalala.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mnazi,Bahati Lusekolo amesema,ujio wa mradi wa Miji 28 utasaidia kuondoa changamoto ya maji wilayani Chunya.

“Tunamshukuru Mbunge wetu kwa jitihada ambazo amekuwa akifanya katika harakati za kuhakikisha wilaya hii inakuwa na maji ya kutosha,hivyo tuendelee kumpa ushirikiano,”amesema Lusekolo.