August 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IFM yawafunza vijana kujiajiri kuunda ajira

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza

CHUO cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kimesema elimu ya juu haipaswi kuishia kumpa kijana cheti, bali kumjengea uwezo wa kutumia maarifa na ujuzi kujiajiri,kuzalisha ajira na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Akizungumza Agosti 8,2026,katika banda la chuo hicho kwenye kilele cha maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliofanyika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Mkuu wa Utawala wa IFM, Kampasi ya Mwanza Dkt.Lawrence Joseph amesema,chuo hicho kimeweka mkazo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa ubunifu na ujasiriamali sambamba na taaluma wanazosoma.

Mkuu wa Utawala Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kampasi ya Mwanza,Dkt. Lawrance Sunga, akionesha baadhi ya bidhaa zilizobuniwa na kutengenezwa na wanafunzi wa chuo hicho, kwa kutuma malighafi mbalimbali za ndani

“Chuo cha IFM kimejikita katika ufundishaji,utafiti na ushauri wa kitaalamu,kinatoa programu za diploma,shahada za kwanza na za uzamili.Kinataka wanafunzi wake wahitimu wakiwa na uwezo wa kutumia taaluma zao katika mazingira halisi ya kazi,biashara na uzalishaji badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee,” amesema Dkt.Sunga .

Amesema wanafunzi chuoni mbali na masomo ya taaluma hufundishwa ujuzi na ubunifu unaowawezesha kubuni bidhaa na huduma zinazoweza kutatua changamoto za jamii,huku baadhi yao wakifanikiwa kuanzisha shughuli za uzalishaji zikiwemo bidhaa za mapambo ya ndani,mafuta ya kupaka na vifaa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt.Sunga,ubunifu uliofanywa na wanafunzi ni jiko linalotumia mafuta machafu lita moja kwa siku,limelenga kutumia nishati hiyo kwa ufanisi huku likisaidia katika utunzaji wa mazingira,likiwa mfano wa namna elimu ya ubunifu inavyoweza kugeuza changamoto za mazingira kuwa fursa za kiteknolojia na kiuchumi.

“Tunawafundisha wapate “skills” (ujuzi) na ubunifu kwa mwanafunzi kutengeneze kitu( bidhaa) kwa kutumia malighafi zilizopo.Tunatoa elimu ya “competence” ili mwanafunzi atoke akiwa na “skills” za maisha,aweze kutengeneza bidhaa za kusaidia watu,” amesema Mkuu huyo wa Utawala.

Ameongeza kuwa wanafunzi hupewa “assignments” zinazowataka kubuni vitu mbalimbali, huku baadhi yao wakifanikiwa kutengeneza programu za kompyuta za kusaidia kufanya hesabu (stocktaking), hatua inayowajengea uwezo wa kutumia teknolojia kutatua changamoto za biashara.

Pia amesema,mfumo huo wa elimu unalenga kuhakikisha mhitimu anatoka chuoni akiwa na zaidi ya cheti cha kitaaluma,kwani anapaswa kuwa na uwezo wa kutumia maarifa yake katika kujiajiri na kutoa huduma kwa jamii.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze, wakiwa katika banda la IFM Kampasi ya Mwanza, wakati wa maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi, kwenye viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza

Kwa mantiki hiyo, IFM imeendelea kuunganisha mafunzo ya darasani na ujuzi wa vitendo, ubunifu na ujasiriamali ili kuwasaidia vijana kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira nchini.

“Fursa hizo zinaendana na mahitaji ya dunia ya sasa ambayo inazidi kutegemea teknolojia katika uzalishaji, biashara, huduma za fedha na mawasiliano. Programu hizi zinaongeza wigo wa taaluma zinazopatikana chuoni, sambamba na dhamira ya taasisi ni kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya jamii na soko la ajira,” amesema Dkt.Sunga.

Aidha, taaluma hizo ni muhimu katika kujenga wataalamu wenye uwezo ili kukidhi mahtaji ya soko na kufanya uchambuzi wa hatari, kusimamia masuala ya fedha, uhasibu, uchumi, benki, bima , teknolojia, usimamizi wa kodi na kutumia takwimu na maarifa ya kifedha katika kufanya maamuzi ya kitaalamu.