

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amempongeza kijana mbunifu wa zana za kilimo, Innocent Mabilika, kwa jitihada zake za kubuni mashine zinazolenga kurahisisha shughuli za wakulima na kupunguza gharama za uzalishaji.
Dkt. Nungu alitoa pongezi hizo katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji ya Nane Nane yaliyohitimishwa jana, Agosti 8, mwaka huu, ambapo alikagua mashine mbalimbali zilizobuniwa na Mabilika.
Alisema Serikali kupitia COSTECH na taasisi nyingine imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana wenye ubunifu, huku akieleza kuwa Mabilika tayari ameonesha uwezo mkubwa kwa kutengeneza mashine zinazotumika na baadhi kuuzwa nje ya nchi.
Dkt. Nungu alisema Mabilika aliwasilisha ombi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, mwezi Juni mwaka huu, akiomba kupatiwa fursa ya kuongeza elimu na ujuzi ili aweze kuboresha zaidi kazi zake za ubunifu.
Alisema Waziri Mkenda alitoa maelekezo kwa Mabilika kupatiwa mafunzo maalumu kupitia taasisi husika, hatua ambayo COSTECH imeanza kuifanyia kazi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Pamoja na ubunifu alionao na kazi kubwa anayofanya, elimu yake ni ndogo ,ameomba apate nafasi ya kuongeza ujuzi ili aweze kufanya kazi kubwa zaidi,” alisema Dkt. Nungu.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwashika mkono vijana wenye ubunifu na kuwasaidia kugeuza mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zinazoweza kuchangia maendeleo ya Taifa.
Dkt. Nungu pia alisema Mabilika anaweza kunufaika na fursa mbalimbali za kifedha zilizopo kwa wabunifu, ikiwamo mifuko inayolenga kuwawezesha vijana kupata vifaa na mitaji ya kukuza uzalishaji.
Alieleza kuwa COSTECH inaendelea kushirikiana na taasisi nyingine kuwezesha wabunifu kupata dhamana na usaidizi wa kifedha kulingana na mahitaji ya kila mbunifu.
“Ukimwambia kampuni yake inahitaji vifaa vya takribani Sh milioni 100, tunamwelekeza kwenye mfuko husika ili aweze kusaidiwa kupata vifaa na kuendeleza uzalishaji,” alisema.
Dkt. Nungu alisema Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya kuwafikia wabunifu nchini, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa madawati katika halmashauri kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili vijana wasiokuwa katika maeneo makuu ya mijini waweze kupata huduma kwa urahisi.
Alisema pia kuna ushirikiano na vyuo vya ufundi ikiwamo VETA, kwa lengo la kuwafikia vijana wenye vipaji na ubunifu wanaotoka katika mifumo isiyo rasmi ya elimu.
Aliwataka vijana wenye ubunifu nchini kutokata tamaa, akisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha ili wabunifu hao waweze kutumia vipaji vyao kutengeneza ajira na kuongeza uzalishaji nchini.
Kwa upande wake,Innocent Mabilika, mwenye umri wa miaka 26, alisema amejikita katika kubuni na kutengeneza zana mbalimbali za kilimo zinazolenga kurahisisha kazi za wakulima na kupunguza gharama za uzalishaji.
Alisema alianza safari yake ya ubunifu mwaka 2014 akiwa shule ya msingi Kibumba, ambako alianza kutengeneza vitu kwa kutumia udongo kabla ya kuhamia kwenye plastiki na baadaye chuma.
“Mwaka 2020 nilipoingia sekondari niliendelea na ubunifu wangu. Baada ya kumaliza kidato cha nne niliingia rasmi katika utengenezaji wa mashine kwa kutumia chuma,” alisema.
Mabilika alisema hadi sasa ametengeneza mashine mbalimbali, ikiwamo mashine za kuvuna mazao, zana za kupanda, mashine za kulima pamoja na matrekta madogo ambayo baadhi yake tayari yanatumiwa na wateja.
Alisema ametengeneza pia mashine za kuvuna aina ya harvester na combine harvester, ambazo baadhi tayari ziko kwa wateja na zinafanya kazi.
Kwa mujibu wa Mabilika, matrekta yake madogo yanauzwa kwa bei zinazofikia Sh milioni nane hadi Sh milioni 12, kutegemea aina na uwezo wa mashine.
Mbunifu huyo alisema katika safari yake ya ubunifu ameshawahi kuwafundisha vijana 16, huku akiwa ameajiri vijana wanne wenye elimu ya shahada wanaomsaidia katika michoro, masoko na shughuli nyingine za kampuni.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni ukosefu wa mitambo na vifaa muhimu vya uzalishaji kutokana na uhaba wa mtaji.
Alitaja baadhi ya vifaa anavyohitaji kuwa ni mashine za CNC na sheet bending machine, ambazo, kwa mujibu wake, zingemsaidia kuongeza kasi ya uzalishaji na kuboresha ubora wa bidhaa zake.
Mabilika aliiomba Serikali, kupitia COSTECH na taasisi nyingine zinazohusika na kuwawezesha wabunifu, kumsaidia kupata vifaa hivyo ili aweze kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa kuagiza baadhi ya mashine kutoka nje ya nchi.
Alisema uwekezaji katika wabunifu wa ndani unaweza kusaidia Serikali kupunguza uagizaji wa zana za kilimo kutoka nje na badala yake kutoa nafasi kwa wazawa kuzalisha mashine hizo hapa nchini.
“Natamani Serikali iwaamini wabunifu wa ndani ili tuweze kufanya biashara kwa mapana zaidi. Ubunifu wangu si wa kitu kimoja; nina uwezo wa kutengeneza vitu mbalimbali vinavyoweza kusaidia wakulima na pia kutoa ajira kwa vijana,” alisema.
Mabilika alisema tayari COSTECH imemsaidia katika suala la elimu, ambapo amepata fursa ya kusoma kozi maalumu katika chuo nchini, hatua anayotarajia itamuongezea ujuzi na uwezo wa kuboresha zaidi ubunifu wake.
Alisema lengo lake ni kuona Tanzania inakuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza zana zake za kilimo ndani ya nchi, huku vijana wakipata fursa za ajira kupitia viwanda na kampuni zinazozalisha teknolojia hizo.

More Stories
Wakulima Mbarali watakiwa kutanua Kilimo cha Korosho
IFM yawafunza vijana kujiajiri kuunda ajira
Waandaaji wa maonesho watakiwa kufuata taratibu