September 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc Shaka aongoza usafi Stendi Kuu Kilosa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MACHO ya abiria na wafanyabiashara katika Stendi Kuu ya Mabasi Kilosa leo asubuhi yaligeuka ghafla kuona jambo ambalo hawakulitarajia. Sio basi jipya lililowasili, bali ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, akiwa na glavu nyeupe mikononi, gunia kubwa begani na ufagio, anaongoza zoezi la usafi kwa vitendo.

Shaka alionekana mstari wa mbele, akiokota taka na kuzibeba mwenyewe huku mamia ya wananchi, mama ntilie, madereva wa bodaboda, maafisa na wapiganaji wa vyombo vya ulinzi na usalama, watumishi wa Idara na taasisi za serikali wakimfuata nyuma kwa hamasa kubwa.

Zoezi hilo lilianza alfajiri katika eneo la soko na stendi, ambapo taka zilizokuwa zimejaa pembeni ya maduka, mitaro iliyoziba na uchafu wa mifuko ya plastiki vimeondolewa na kupakiwa kwenye gari la Halmashauri.

Akizungumza kwa hisia na msimamo mkali mara baada ya zoezi hilo, Shaka alisema:

“Leo hatujaja kupiga picha. Tumeamua kutoka ofisini kuja mtaani kufanya usafi kwa vitendo, sio kwa maneno. Kiongozi lazima aongoze kwa mfano, na ndio maana mnaniona na glavu mkononi.”

“Stendi yetu, Soko letu ndio sura ya Wilaya yetu. Mgeni akiteremka kwenye basi akakutana na uchafu, atasema Kilosa yote ni chafu. Hii sura lazima tuibadilishe. Hatuwezi kukubali Kilosa iitwe chafu.”

“Usafi ni afya, usafi ni heshima, usafi ni uchumi. Tumeanza hapa Stendi, lakini usafi huu uendelee katika maeneo yote ya umma na hata majumbani kwetu binafsi. Kila mwananchi awe balozi wa usafi.”

Katika hatua madhubuti zaidi, Shaka ametoa agizo kali kwa watendaji wa Halmashauri:

“Nimeagiza Halmashauri, kuanzia kesho kila mfanyabiashara awe na dumu la taka mbele ya biashara yake. Hili sio ombi, ni agizo. Asiyefanya hivyo, sheria itachukua mkondo wake. Tutachukua hatua stahiki kwa wale wote watakaokaidi suala la usafi. Hakuna mjadala kwenye hili.”

Wananchi walioshiriki zoezi hilo wamepongeza hatua hiyo, wakisema ni mara chache kuona kiongozi wa Wilaya akishiriki usafi kwa kujishusha kiasi hicho, na kumpongeza kwa uongozi wa mfano.