September 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakenya,Watanzania watawala Yas Zanzibar International Marathon

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Onine

WANARIADHA wa Kenya wametawala mbio za kilomita 21 za Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku Watanzania waking’ara katika mbio za kilomita 10 kwenye msimu wa sita wa mashindano hayo, yaliofanyika jana kwenye Viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Katika kilomita 21 kwa wanaume, Wakenya Justus Nyesya, Ransisi Kamito na Simon Kelenzyo walishika nafasi tatu za juu mtawalia. Kwa wanawake, Valentine Chep na Rael Mitieka wa Kenya walimaliza nafasi ya kwanza na pili, huku Mtanzania Failuna Abdi akishika nafasi ya tatu.

Kilomita 10 kwa wanaume ilitawaliwa na Watanzania Shedrak Damas na Boay Maganga waliomaliza nafasi ya kwanza na pili, huku Duncan Kipchumba wa Kenya akiwa wa tatu. Kwa wanawake, Mkenya Faith Jeptum alishinda, akifuatiwa na Watanzania Anna Dolomong na Dorcas Boniface.

Mbio hizo za kilomita 21, 10 na 5 ziliwakutanisha wanariadha kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma, aliyemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amewapongeza wanariadha, waandaaji na wadhamini kwa kuendelea kukuza mbio hizo na kuitumia michezo kuitangaza Zanzibar.

“Mashindano haya yana mchango mkubwa katika kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kama moja ya maeneo muhimu ya utalii. Tunapowakaribisha wanariadha na wageni kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali, tunafungua pia fursa kwa sekta nyingine ikiwemo hoteli, usafiri, biashara na huduma mbalimbali zinazowanufaisha wananchi wetu,” amesema Juma.

Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa michezo katika kuendeleza matukio yenye mchango katika kukuza utalii, kuhamasisha afya na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura, amesema katika kipindi cha miaka sita, Yas Zanzibar International Marathon imeendelea kukua kutoka kuwa mashindano ya mbio pekee na kuwa jukwaa linalochangia kuitangaza Zanzibar kupitia michezo na utalii.

“Kwa miaka sita sasa, Yas Zanzibar International Marathon imekuwa zaidi ya mbio. Imekuwa sehemu muhimu ya kuitangaza Zanzibar kwa kuwakutanisha Wazanzibari na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania, kuhamasisha mtindo bora wa maisha, kutangaza vivutio vya utalii na kuchochea uchumi wa buluu,” amesema Rwetabura.

Amesema, Yas na Mixx zinajivunia kuwa sehemu ya safari hiyo sambamba na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika mawasiliano na huduma za kidijitali Zanzibar.

Kwa mujibu wa Rwetabura, mtandao wa Yas kwa sasa umeenea kwa takriban asilimia 99 Zanzibar, huku uwekezaji wa teknolojia ya 4G ikiwa ndio ya chini na uwekezaji wa 5G ukiendelea katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.