September 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watarajiwa fidia stahiki North Mara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Mara

BAADHI ya  wananchi wa Kijiji cha Matongo hususani wakazi wa Vitongoji vya Nyamilama na Masangula mkoani Mara, wameeleza matumaini yao ya kupata fidia stahiki katika zoezi la tathmini ya mali na maeneo yanayohusishwa na shughuli za mgodi wa Barrick North Mara.

Wakizungumza wananchi hao ambao  watapisha ujenzi wa bwawa la majitaka (Tailings Storage Facility- TSF) katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara walisema,tathmini hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha ardhi,nyumba,miti na mali nyingine zinazoweza kuathiriwa na shughuli za mgodi zinatambuliwa na kupewa thamani inayostahili kabla ya maeneo yao kupisha shughuli za mradi.

Ambapo tayari watu zaidi ya 350 wamefanyiwa uthamini wa mali zao ili waweze kulipwa fidia kupisha eneo linalohitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.

Mkazi wa Kitongoji cha Nyamilama, Pius Ijukaine amesema,zoezi hilo linaendelea vizuri na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na wahusika ili mchakato huo ukamilike kwa amani na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.

“Ninamiliki eneo lenye miti ya mikaratusi,natarajia thamani ya miti hiyo kuzingatiwa wakati wa tathmini na mchakato wa fidia.Naiomba Barrick North Mara kuangalia uwezekano wa kuwapatia maeneo mengine wananchi ambao watapaswa kuondoka au kupisha maeneo yao kwa ajili ya shughuli za mgodi,”amesema Ijukaine.

Kwa upande wake, Elias Daniel, mkazi wa Kitongoji cha Nyamilama, amesisitiza umuhimu wa fidia kutolewa kwa usahihi kwa wananchi wenye ardhi na mali zinazoweza kuathiriwa na shughuli za mgodi,kwani wanategemea ardhi zao kwa shughuli mbalimbali za kilimo na uzalishaji.

Naye Zubeida Saidi, mkazi wa Kitongoji cha Masangula amesema,wananchi wanahitaji uhakika kwamba mchakato wa malipo ya fidia utasimamiwa vizuri na kwa kuzingatia stahiki za kila mwananchi anayehusika huku akiomba mgodi uwapatie fedha  itakayokidhi thamani ya maeneo waliowapatia.

Saidi amesema,ni muhimu wananchi kupewa taarifa sahihi kuhusu hatua zinazofuata katika mchakato huo, ikiwemo namna thamani ya ardhi na mali nyingine itakavyobainishwa na utaratibu wa malipo ya fidia,kwani wanahitaji kuona mchakato huo ukienda kwa uwazi.

 Hata hivyo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamilama, Wambura Chacha amesema,wananchi wanatarajia kupata fidia itakayolingana na thamani halisi ya maeneo na mali zao.Huku ushirikishwaji wa wananchi katika hatua mbalimbali za mchakato ni muhimu ili kujenga uelewa na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa zoezi hilo.

Hivyo amewataka wananchi kuendelea kuheshimu tamko la Serikali la kutokuendelea na ujenzi au shughuli zinazohusiana na mradi katika maeneo husika wakati mchakato wa tathmini na hatua nyingine ukiendelea.Ambapo amewasisitiza kuwawatulivu na kushirikiana na viongozi pamoja na wataalamu wanaohusika ili zoezi hilo lifanyike kwa utaratibu na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.