Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Igunga
MIRADI ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 wilayani Igunga mkoani Tabora imekaguliwa,kuwekewa jiwe la msingi na kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda.
Akiongea na wananchi katika maeneo mbalimbali ambako Mwenge huo umepita Kiongozi huyo ameishukuru Serikali kwa kuleta mabilioni ya fedha katika wilaya hiyo.

Amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru umeridhika na kazi iliyofanyika kwenye utekelezaji miradi ya wananchi ndio maana ameweka jiwe la msingi na kuzindua miradi yote kwa sababu imejengwa kwa ubora unaotakiwa.
“Nakupongeza sana Mkuu wa Wilaya Sauda Mtondoo,Mkurugenzi Mtendaji Selwa Hamid na Wataalamu wote kwa kusimamia vizuri na kwa dhati fedha zilizoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hii,” ameeleza.
Miradi iliyotembelewa na kuzinduliwa na Kiongozi huyo ni mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliojengwa katika Shule ya Sekondari Ziba ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo kwa jamii, wenye thamani ya sh.mil 14.4.
Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na kuwa mkombozi kwa wananchi kwa sababu umesaidia kupunguza uharibifu wa mazingira, kuhifadhi misitu, kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha afya ya jamii.
Mingine ni mradi wa kiuchumi wa Kikundi cha Vijana Wajasiriamali cha Faraja kutoka Kata ya Igurubi ambacho kimewezeshwa na halmashauri mkopo nafuu usio na riba wa sh. mil 30 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Mradi mwingine ni ujenzi wa madarasa 6, mabweni 2 na matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Choma uliogharimu kiasi cha sh.mil 450, mradi huu umekamilika kwa asilimia 95 na kuleta tija kubwa kwenye ufaulu wa wanafunzi.
Mradi wa upanuzi Kituo cha afya Chomachankola ambapo majengo 4 yamejengwa ikiwemo wodi ya mama na mtoto, maabara, jengo la wagonjwa wa ndani na jengo la ufuaji ambayo yamegharimu kiasi cha sh mil 683.5.

Mradi wa ujenzi wa daraja la mawe lenye urefu wa mita 25.5 linalounganisha Kata za Choma na Nyandekwa ambalo limegharimu kiasi cha sh.milioni 203.8 na limekamilika kwa asilimia 100, daraja hili limemaliza kilio cha miaka mingi.
Mradi wa kiwanda binafsi cha kuchenjua dhabahu ambapo yamejengwa mabwawa ya kuhifadhi mabaki ya uchakataji dhahabu, mradi huu wa uwekezaji uliogharimu sh.bil 1.01 umeleta neema kubwa wachimbaji wadogo.
Na mradi wa upanuzi wa maji ya Ziwa Victoria wa ujenzi wa matanki 2 ya maji katika Hospitali ya Rufaa Nkinga ili kuboresha upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Kata ya Ziba na maeneo jirani uliogharimu sh.bil 2.48.



More Stories
TANESCO yatakiwa kuongeza ubunifu katika utafiti na mipango
Wananchi watarajiwa fidia stahiki North Mara
Wakenya,Watanzania watawala Yas Zanzibar International Marathon