August 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ujenzi wa Barabara ya Kahama

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kiserikali,Deogratius Ndejembi, amemtaka Mkandarasi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola, M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi kuanza kunufaika na miundombinu hiyo.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo, Agosti 9, 2026, mkoani Shinyanga, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 73 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema hadi sasa kilomita 32 kati ya 73 zimekamilishwa kwa kuwekwa lami, huku kazi nyingine za ujenzi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi.

“Sina mashaka na ubora wa kazi inayofanywa na Mkandarasi, lakini anatakiwa kuongeza kasi ili barabara ikamilike kwa wakati. Wananchi wanataka kuona barabara yao inakamilika na kuanza kuitumia,” amesema Ndejembi.

Amesisitiza kasi ya utekelezaji inapaswa kuendana na ubora wa kazi, akieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo inayopitia.

Aidha,Ndejembi ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga kumsimamia kwa karibu Mkandarasi huyo na kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaongezeka ili mradi ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa watumiaji wa barabara kwa kuhakikisha barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinawekewa taa za barabarani, hususan katika maeneo yenye shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi.

Amesema uwekaji wa taa hizo ni sehemu ya maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, kwa lengo la kuimarisha usalama na kuwezesha wananchi kutumia barabara kwa usalama zaidi nyakati za usiku.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mboni Mhita, amesema Serikali imetoa zaidi ya Shilingi trilioni 2 kwa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati huku akiahidi kusimamia kwa karibu ujenzi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola ili fedha zilizotolewa na Serikali na maelekezo ya Rais yatekelezwe kwa wakati.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema ujenzi wa Barabara ya Kahama – Bulyanhulu Jct–Kakola wenye urefu wa kilomita 73 unagharimu Shilingi bilioni 100.6.

Amesema mradi huo ulipangwa kukamilika mwezi Septemba 2026, hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, Mkandarasi ameomba kuongezewa muda wa kukamilisha kazi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mwaikokesya, iwapo muda wa nyongeza utaidhinishwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026.