Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
TAASISI ya Self Microfinance Fund imeweka mkazo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kuwawezesha wananchi kupata mikopo itakayosaidia kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza thamani ya bidhaa na kuwaunganisha na fursa za masoko.
Ofisa Mikopo wa Taasisi ya Self Microfinance Adolf Itinde,amesema hayo Agosti 8,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la taasisi hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi, yaliyofanyika katika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Amesema Self Microfinance Fund ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inayotoa elimu ya fedha na mikopo,mikopo na huduma mbalimbali za bima zikiwemo bima ya moto, maisha na kilimo,ambayo inatoa mikopo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo,biashara,viwanda na usafirishaji.
Itinde amesema ili kupata mkopo, mwombaji lazima awe Mtanzania anayefanya shughuli halali hapa nchini, huku biashara yake ikiwa imefanya kazi kwa angalau miezi 12, akiwa na historia nzuri ya ukopaji na urejeshaji pamoja na kuwa na dhamana.Pia mikopo hiyo hutolewa kwa viwango vya chini, kati na juu ikiwemo kwa shughuli za kilimo cha mazao na ufugaji.
Hata hivyo amesema mchango wa taasisi hiyo katika Dira ya Taifa 2050 unatokana na mikopo inayowezesha wananchi katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji, uchakataji,usafirishaji,uhifadhi,pmatumizi ya teknolojia hadi masoko, hatua inayolenga kuongeza tija na thamani ya bidhaa za wananchi.
Sanjari na hayo Itinde amesema taasisi hiyo yenye matawi 12 hapa nchini, katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 50, huku kwa tawi la Mwanza likilenga kutoa zaidi ya sh bilioni 8 na kuwafikia watu takribani 200.
Hivyo amesisitiza kuwa kabla ya kutoa mkopo,taasisi hiyo utoa elimu ya fedha na mikopo kwa waombaji,hivyo aliwahimiza vijana ambao bado hawajaanza biashara kufika katika ofisi za taasisi hiyo kupata elimu na maandalizi ya mikopo wakati wakisubiri kutimiza vigezo.
Akizungumzia fursa ya ufugaji wa kuku, Itinde amesema soko la Mwanza lina uhitaji wa kuku na mayai, hivyo wafugaji wanaofuga kuanzia kuku 100 wanaweza kufika katika ofisi za taasisi hiyo kuomba mikopo baada ya kukidhi, huku akiwahimiza wakazi wa Mwanza kutumia fursa hiyo kupanua biashara na kuongeza uzalishaji.
Amewahimiza Watanzania kutembelea ofisi za Self Microfinance Fund kupata elimu ya fedha,mikopo na bima, akisisitiza kuwa uwezeshaji huo unalenga kuwasaidia wananchi kukuza shughuli zao za kiuchumi, kuongeza kipato na hatimaye kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Mwishoo

More Stories
Wananchi watakiwa kutunza,kulinda barabara
Benki 21 zimewezeshwa na TADB kuwakopesha wakulima wadogo
Ndejembi amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ujenzi wa Barabara ya Kahama