Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
WATU 10 mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu na utapeli kupitia ahadi za ajira na biashara.
Akizungumza Julai 18,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa,amesema Julai 16,2026, majira ya saa 4:30 asubuhi, katika mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma wilayani Nyamagana mkoani humo,jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Ukamataji huo ulitokana na taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu
uwepo wa kikundi cha wahalifu ambao wamekuwa wakiwashawishi wananchi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Geita, Kigoma,Kagera,Tabora,Morogoro na maeneo mengine nchini,kufika mkoani Mwanza kwa madai ya kupatiwa ajira na fursa za biashara kupitia kampuni. inayojitambulisha kama “Alliance In Motion Global”.
DCP.Mutafungwa amedai kuwa baada ya waathirika wa matukio hayo kusafirishwa kutoka maeneo mbalimbali
na kufikishwa mkoani Mwanza, wamekuwa wakitozwa fedha kwa madai ya kusajiliwa kwenye biashara, huku fedha nyingine wakitozwa kwa ajili ya kupewa mfumo wa kuanza kufanya
biashara.
Hata hivyo, baada ya kulipa fedha hizo, wengi wao walijikuta hawajapatiwa
huduma wala fursa walizoahidiwa na hivyo kuibiwa fedha zao.
Ambapo watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ambao ndiyo viongozi wa kampuni ya “Alliance In Motion Global” Mwanza ni Athuman Hamisi(29),ambaye ndiye kiongozi mkuu wa kampuni hiyo.
Emmanuel Manyau(27),Avison Mwemezi(23),Justine Joseph(23), Stephano Laurent(23),Tinalile Andrew(23),Fraison Lufungulo(24), Happyness Henry(23),Peter Kiyombi(54) mchungaji wa kanisa na Adriano John(40) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma Kati.
Hata hivyo amesema,jeshi hilo linaendelea na mahojiano ya kina na watuhumiwa hao ili kubaini mtandao
mzima wa uhalifu huo pamoja na kuwakamata wahusika wengine wanaohusika na shughuli
hizo.
Aidha amesema,hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika mara
baada ya uchunguzi kukamilika.Huku akitoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapopewa ahadi za ajira au biashara zinazowataka kutoa fedha kabla ya kupata huduma au fursa hizo.
“Nawashauri wananchi kuthibitisha uhalali wa kampuni au taasisi yoyote kabla ya kujiunga nayo au kutoa fedha ili kuepuka kuingia mikononi mwa matapeli wenye tamaa za fedha kisha kuibiwa,”amesisitiza DCP.Mutafungwa.

More Stories
Watuhumiwa kumshambulia mzee kisa imani za kishirikina
Upatikanaji wa maji Chunya wafikia asilimia 52
MiXX Yakabidhi Zawadi kwa Washindi wa Kampeni ya Kombe la Dunia