Na Joyce Kasiki, Dodoma
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imetumia teknolojia ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kubaini visumbufu vya mazao katika mashamba ya wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma, hatua inayolenga kuwezesha udhibiti sahihi na endelevu wa magonjwa na visumbufu vya mimea.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada yabkuhitimishwa maonyesho ya Wakulima na wafugaji katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Profesa Joseph amesema, sampuli za mazao mbalimbali, yakiwemo mihogo, vitunguu, karanga, sukuma wiki, Chinese na beetroot, zilikusanywa katika maeneo ya uzalishaji Mpwapwa na kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia teknolojia ya DNA.
Amesema teknolojia hiyo imewezesha kubaini visumbufu ambavyo wakati mwingine haviwezi kuonekana kwa macho, hivyo kuwasaidia wataalamu na wakulima kuchagua njia sahihi za udhibiti pamoja na viuatilifu vinavyolenga kisumbufu husika.
“Lengo ni kwamba kama ni bakteria ambao udhibiti wake unahitaji kutumia kiuatilifu, tutakwenda na kiuatilifu sahihi, sio tena kukisia-kisia,” amesema Profesa Ndunguru.
Kwa mujibu wa Profesa Ndunguru, katika zao la mihogo vilibainika visumbufu mbalimbali, vikiwemo utitiri, bakteria na fangasi, ambavyo baadhi yake vinaweza kudhoofisha mmea na kuongeza uwezekano wa kushambuliwa na vimelea vingine.
Katika zao la vitunguu, uchunguzi ulibaini visumbufu nane vilivyohusisha mchanganyiko wa bakteria na fangasi. Amesema teknolojia hiyo pia iliwezesha kubaini uwepo wa vimelea hata katika mimea ambayo haikuwa imeonyesha dalili zinazoonekana kwa macho.
“Uzuri wa teknolojia hii ni kwamba hata kama kuna kisumbufu ndani ya mmea na mmea hauonyeshi dalili yoyote, teknolojia hii inaweza kukuonyesha kwamba kisumbufu hicho kipo,” amesema.
Amesema uwezo huo ni muhimu katika kuzuia kuenea kwa magonjwa, hususan katika mbegu na mazao yanayosafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine.
Kwa upande wa karanga, visumbufu vitatu vilibainika, ikiwemo virusi vinavyosambazwa na vidukari na vinavyoweza kuathiri ukuaji wa mmea kwa kusababisha majani kuwa ya njano na mmea kudumaa.
Katika zao la Chainizi alisema, uchunguzi ulibaini visumbufu sita, vikiwemo bakteria na fangasi wanaoweza kusababisha uozo na kuathiri uzalishaji. Aidha, katika sukuma wiki vilibainika visumbufu vitatu bakteria, fangasi na virusi.
Profesa Ndunguru amesema matokeo hayo yataisaidia TPHPA kuandaa mpango wa udhibiti wa visumbufu kwa kuzingatia aina ya kisumbufu na eneo kilipo.
Amesema iwapo uchunguzi huo utafanyika katika maeneo mbalimbali nchini, Tanzania inaweza kuwa na ramani inayoonyesha mtawanyiko wa visumbufu vya mazao, jambo litakalowezesha usambazaji wa viuatilifu kwa utaratibu wa kimkakati.
“Unapeleka kiuatilifu sahihi katika eneo sahihi kudhibiti aina sahihi ya kisumbufu ambacho tumekibaini,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya viuatilifu yatasaidia kupunguza gharama kwa wakulima, madhara kwa mazingira na uwezekano wa visumbufu kujenga usugu dhidi ya viuatilifu.
Profesa Ndunguru amesema uchunguzi huo ukipanuliwa nchini kote utawezesha Tanzania kuwa na ramani ya kitaifa ya visumbufu vya mazao, jambo litakalosaidia kupanga mikakati madhubuti ya kudhibiti magonjwa, kuongeza tija katika kilimo na kuboresha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje.
Amesema udhibiti bora wa visumbufu utaongeza uzalishaji, kuchangia ajira na kukuza uchumi wa nchi.
“Sayansi, teknolojia na ubunifu ni nyenzo muhimu ya kusukuma uchumi wa nchi yoyote,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Salum Ally, amesema matumizi ya teknolojia hiyo yamewasaidia wataalamu kubaini changamoto ambazo hapo awali zilitegemea zaidi uchunguzi wa macho na uzoefu wa misimu iliyopita.
Amesema wakulima wamekuwa wakitumia dawa kwa kuzingatia changamoto walizokutana nazo katika misimu iliyopita, hali ambayo wakati mwingine inaweza kusababisha matumizi ya tiba isiyolenga kisumbufu kilichopo.
“Unaweza ukatibu tatizo moja lakini bado ukaendelea kupata matatizo mengine. Kupitia kipimo hiki sasa kinatupa mwangaza wa kutatua matatizo yanayowakabili wakulima,” amesema Ally.
Ally ameitaka TPHPA kuendelea kusogeza teknolojia hiyo kwa wakulima wengi zaidi ili waweze kupata taarifa sahihi kuhusu visumbufu vilivyopo katika mazao yao na kutumia njia stahiki za udhibiti.
Amesema upatikanaji wa taarifa sahihi za visumbufu ni muhimu katika kumsaidia mkulima kuzalisha katika mazingira salama, kuongeza tija na kuboresha kipato kutokana na kilimo.

More Stories
Wazazi wahimizwa kuwekeza elimu yenye maadili, hofu ya Mungu na vipaji kwa watoto
Msajili wa Hazina ateta na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo
Rushwa yatakiwa kukomeshwa kabla watoto hawajajifunza kuipenda