July 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakuu wa shule 49 Zanzibar watembelea Paradise Mission

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Mbeya

SHULE ya Paradise Mission iliyopo Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, imepokea ugeni wa wakuu wa shule 49 kutoka Zanzibar waliotembelea taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujionea mbinu mbalimbali zinazotumika kuimarisha ubora wa elimu.

Akizungumza wakati wa kuwapokea wageni hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Paradise Mission, Ndele Mwaselela, amewapongeza kwa kuchagua kutembelea shule hiyo, akieleza kuwa ziara za kujifunza ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu na kuinua viwango vya ufundishaji nchini.

Mwaselela amewahimiza wakuu hao wa shule kuendelea kubadilishana uzoefu, mawazo na mbinu bora za ufundishaji pamoja na uongozi wa shule, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utachangia kuongeza ubora wa elimu na kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia.

“Ninaamini maarifa na uzoefu mtakaobadilishana kupitia ziara hii yatachangia kuimarisha utendaji wa shule zenu na kuinua kiwango cha elimu kwa ujumla,” amesema Mwaselela.

Kwa upande wao, wakuu hao wa shule kutoka Zanzibar walieleza kufurahishwa na mapokezi waliyopata pamoja na fursa ya kujifunza mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa shule, mbinu za ufundishaji na usimamizi wa elimu zinazotumiwa na Paradise Mission.

Walieleza kuwa maarifa waliyopata yatawasaidia kuboresha utendaji wa shule wanazoziongoza na kuongeza ubora wa utoaji wa elimu Zanzibar, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano na Paradise Mission kwa manufaa ya sekta ya elimu nchini.

Mkuu wa msafara wa wakuu wa shule kutoka Kusini Unguja ,Shekhe Othman Ussi amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kuona utofauti sehemu waliyotoka .

“Tumejifunza vitu vingi sanaa na tunaahidi ushirikiano wa kutosha katika kuyafikia malengo ya kunyanyua taarifa kwa watoto wetu kwani maarifa tuliyoona hapa ni ya kiwango cha juu “amesema Mwl.Ussi.