April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu waeleza lishe inayofaa kipindi cha mfungo wa Ramadhan

Na Aveline Kitomary,TimesMajira online,Dar es Salaam.

KIPINDI cha mwezi wa Mtukufu wa Ramadhan familia nyingi za imani ya kiislamu hufunga saumu ikiwa ni sehemu muhimu ya kutimiza nguzo ya kiislamau.

Kipindi cha mfungo hutimiza siku 30 baada ya hapo hufuata sikukuu ya Iddi.

Baada ya kufunga siku nzima hufungua kwa kula vyakula mbalimbali wakati wa jioni ambavyo huwa ni vingi kuliko siku za kawaida.

Wakati mwingine wanaofuturu hula chakula kingi kupita kiwango cha kawaida bila kujua madhara ya ulaji huo.

Hali ya ulaji wa chakula kingi sio tu hufanya kiwango cha uzito kuongezeka mwezi huu wa Ramadhan bali kwa wa wale walaji ambao wana matatizo mbalimbali ya moyo kama shinikizo la damu la juu (High Blood Pressure), moyo dhaifu (heart failure), moyo uliopanuka (Dilated Cardiomyopathy), mishipa/mirija ya moyo iliyoziba (coronary artery disease CAD) wanaweza kupata matatizo ya kiafya .

Akizungumzi hali hiyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Pro. Mohhamed Janabi, anasema ulaji wa chakula kingi kunaweza kuchochea mstuko wa ghafla wa moyo (trigger heart attack).

“Mstuko wa moyo unasababisha mamilioni ya watu kupoteza maisha kila mwaka duniani na kila mwaka vifo hivi vinaongezeka zaidi duniani kipindi hiki cha Ramadhan na wakati wa sherehe mbalimbali kama vile Krismasi,Pasaka na mwaka mpya.

SABABU YA KUONGEZEKA VIFO

Tafiti zinaonyesha kipindi kama hiki cha Ramadhan vifo vinavyotokana na mstuko wa moyo huongezeka mara nne (4) zaidi.

Prof.Janabi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo anabainisha kuwa kuna sababu kadhaa zinazoweza sababisha kuchochea mstuko wa moyo ambazo ni mtu unapokula chakula kingi mpaka kuvimbiwa wakati wa kufuturu/iftar au wakati wa daku,tumbo la chakula linapanuka ili kupokea chakula hicho.

“Hii itapelekea damu mwilini kujipanga upya kwa kutoa damu nyingi kutoka kwenye moyo kuelekea/ kupelekwa “redistribution”kwenye njia ya chakula “Digestive System” ili kusaidia kusaga “digest” chakula kingi kilicholiwa nyakati za futari/daku.

“Hali hii ikimkuta mlaji ambae ana tatizo lake la moyo au pressure la siku nyingi/zamani kwa mfano mirija au mishipa yake ya damu ya moyo imeziba kidogo au sana huu mbadiliko wa mwendo wa damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye tumbo ndio unapelekea kuchochea “trigger heart attack” ambayo itasababisha mstuko wa moyo na athari zake,”anabainisha Prof. Janabi.

Anafafanua kuwa tumbo lililojaa kutokana na ulaji wa chakula kingi sana husababisha moyo kwenda mbio ‘palpitation’ au mapigo kutokwenda sawa sawa ‘irregular heartbeats’ pia huchochea mstuko wa moyo na wengine kupata kiarusi.

HALI YA MAGONJWA YA MOYO

Prof.Janabi anasema magonjwa ya moyo yanaongoza duniani kwa kusababisha vifo ukilinganisha na magonjwa mengine yeyote.

“Zaidi ya watu milioni 18 hufariki duniani kila mwaka kwa sababu ya magonjwa ya moyo hii ni asilimia 31 ya vifo vyote duniani, kati ya hivi vifo vya moyo asilimia 85 vinatokana na mstuko wa moyo ‘heart attack’.

“Robo tatu (3/4) ya vifo hivi vya moyo vinatokea kwenye nchi zenye uchumi mdogo au uchumi wa kati (low/middle income countries),asilimia 80 ya magonjwa ya moyo yanaweza kukingika (prevented) kwa mfano kuacha uvutaji wa sigara, kula vyakula bora na kwa kiasi (kumbuka bibi zetu walikuwa wanasema usile mpaka uvimbiwe), kupunguza uzito, kufanya mazoezi, kupunguza unywaji wa pombe na mengine.

“Wale waliogundulika na matatizo ya moyo,BP kuwa juu, kisukari, uzito mkubwa ‘overweight na obesity’ kufuata masharti ya madaktari wao,”anasema Prof Janabi.

ASHAURI ULAJI KIASI

Prof.Janabi anashauri watu wanaofunga kula kwa kiasi vyakula ili kuweza kuwa salama katika kipindi cha mfungo na baada ya mfungo.

“Tufungue funga zetu au tule kwa kiasi hasa tule vyakula vyenye protini nyingi kuliko wanga mwingi na hili hasa kwa wale wenye matatizo ya moyo kabla ya mfungo au yamengundulika mwezi huu Kupunguza vyakula vyenye sukari nyingi.

“Ushauri huu wa ulaji wa chakula nimeutoa kwa kila mtanzania.
“Ukiona dalili za tatizo la moyo kuchoka kuliko kawaida ‘fatigue’ shida ya kupumua sawa sawa, kiungulia/maumivu ya chembe ‘heartburn’ na maumivu kifuani.

“Tafadhali tafuta kwa haraka ushauri wa daktari dalili hizi wakati mwingine haziwezi kuondoka zenyewe,”anashauri Prof.Janabi.

LISHE INAYOTAKIWA

Taasisi ya Chakula na Lishe imekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuhamasisha lishe bora hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Hii ni kutokana na lishe kuwa sehemu mhimu katika kubakabilia na magonjwa hasa magonjwa yasiyo ya kumabukiza.

Afisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC, Fatma Mwasora anasema kuwa kama mtu atakula futari,daku ahakikishe chakula hicho kinakuwa ni mlo kamili ambao unatokana na makundi matano ya vyakula.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam,Mwasora anasema kuwa wanasisitiza ulaji huo kwani kumekuwa na tabia katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan watu wengi huwa wanaangalia vyakula kutoka kundi moja ambalo linahusisha vyakula aina ya nafaka na mizizi.

Afisa huyo Mtafiti anafafanua kuwa kwenye kundi la mizizi ni viazi vitamu, mviringo mihogo na ndizi mbichi kisayansi hilo ni kundi moja.

“Hata vile virutunishi ambavyo tunavipata vinatokana na kundi moja hivyo kusababisha hukosekana vingine vinavyotokana na makundi mengine ya vyakula.

“Imekuwa ni mazoea kwa Waislamu katika mfungo akili yetu futari ni lazima iwe ni chakula kinachotokana na mizizi au nafaka,” anasema Mwasora.

Anaongeza kuwa vyakula hivyo mara nyingi vinapoliwa mwili hupata nishati lishe au wanga kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu na joto tu na kukosa virutubishi toka kwenye makundi mengine.

“Vyakula hivi sisi tunaona ndio vyakula vya futari ukiangalia uji unatokana na nafaka, kwenye futari utakuta tambi wakati nayo imetoka katika kundi hilo hilo tunapata virutunishi vya aina moja vya nishati lishe, “anasema mtafiti huyo.

Anasema kuna athari zake iwapo mtu atakula kundi moja la chakula ambavyo ni vyakula vya vinavyotokana na nafaka na mizizi tu, kwani atakosa vyakula vya aina ya Protini, vitamini na madini ambavyo ni muhimu katika kujenga mwili na kuimarisha kinga mwili.

Aidha anawataka Waislamu kula vyakula vinavyotokana na makundi yote matano ili kukamilisha mlo kamili, ambao ni vyakula vya aina ya nafaka, mizizi na ndizi mbichi, jamii ya mikunde na nyama na vile vinavyotokana na mboga mboga na matunda na kwa kiasi vile vinavyotokana na sukari na mafuta.

Futari ni kile chakula au mlo ambao mara nyingi hutayarishwa katika kipindi cha kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani na daku ni mlo ambao hupaswa kuliwa wakati wa usiku kabla ya funga inayofuatia.