June 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanu:Grand Challenges kukuza ubunifu Tanzania

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

SERIKALI imesema uzinduzi wa Mpango wa Grand Challenges Tanzania ni hatua muhimu itakayochochea matumizi ya sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu katika kutafuta suluhisho endelevu za changamoto zinazoikabili nchi.

Aidha, imeeleza kuwa mafanikio ya mpango huo yatapimwa kwa kiwango cha maboresho yatakayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati akizindua rasmi mpango huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ambapo amesema mpango huo unafungua ukurasa mpya wa kuimarisha mchango wa tafiti na bunifu za ndani katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na kujenga mazingira yatakayowawezesha watafiti na wabunifu kutoa majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii.

“Mpango huu unatoa fursa ya kukuza tafiti na bunifu za ndani, kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawanufaisha wananchi moja kwa moja,” amesema.

Aneongeza kuwa kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mshirika wa Jumuiya ya Grand Challenges ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya kimataifa kwa uwezo wa watafiti na taasisi za nchini katika kubuni suluhisho bunifu na endelevu za changamoto za maendeleo.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayochochea ukuaji wa sayansi na teknolojia nchini ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa, hususan katika sekta za afya, kilimo na nishati safi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk. Islam Seif Salum, alisema mpango huo unatoa fursa ya kuelekeza maarifa, tafiti na ubunifu katika kutafuta majawabu ya changamoto za maendeleo zinazohitaji uwekezaji mkubwa katika sayansi na teknolojia.

Amesema Zanzibar imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maeneo ya utafiti na ubunifu, hususan katika uhifadhi wa mazingira ya pwani na bahari, matumizi ya nishati jadidifu pamoja na kuboresha afya ya jamii.

Dkt. Salum amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, akieleza kuwa mafanikio ya Tanzania yatategemea uwezo wa pande zote za Muungano kushirikiana, kubadilishana maarifa na kutumia ubunifu kwa manufaa ya wananchi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia (NFAST), zaidi ya Shilingi bilioni 129 zimehamasishwa kusaidia tafiti, ubunifu, maendeleo ya teknolojia na ujenzi wa miundombinu ya kisayansi.

Amesema kati ya fedha hizo, Serikali imechangia zaidi ya Shilingi bilioni 85, hatua iliyowezesha kuboreshwa kwa maabara za kisasa, kuimarishwa kwa uwezo wa watafiti, kupanuliwa kwa vituo vya ubunifu na kuwapatia vijana fursa za ufadhili wa tafiti pamoja na mafunzo mbalimbali.

Dkt. Nungu amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu yanatafsiriwa kuwa sera, teknolojia na huduma zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, huku zikichangia ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya  Taifa.