Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimeingia makubaliana ya kuwapatia ujuzi waraibu waliopona baada ya kutumia dawa za kulevya.
Lengo likiwa waweze kujitegemea na kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo leo jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.
Amesema, mikakati hiyo ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu katika jamii.

“Ushirikiano na VETA umetokana na kutambua umuhimu wa kuwawezesha waraibu waliopona kupata ujuzi wa kujiajiri na kushiriki shughuli za uzalishaji.
“Pia ushirikiano huu ni mfano mzuri wa namna taasisi za serikali zinavyoweza kushirikiana katika kutatua changamoto za kijamii kwa manufaa ya taifa,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Amefafanua kuwa, waraibu wengi wanaopata nafuu hujikuta wakirejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya endapo hawapati shughuli za kufanya au mbadala wa kuwawezesha kujipatia kipato. Hivyo, mafunzo ya ufundi stadi yatawasaidia kujenga maisha mapya na kuondokana na mazingira yanayoweza kuwarudisha kwenye uraibu.

Aidha, amesema baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wahitimu watawezeshwa vifaa vidogo vya kuanzia kazi kulingana na ujuzi walioupata ili waweze kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato.
Pia, wataunganishwa na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo (microfinance) ili kupata mitaji ya kuanzisha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Kamishina Lyimo amesema ushirikiano huo unaendana na mradi wa serikali wa ujenzi wa kituo kikubwa cha urejeshaji na mafunzo kwa waraibu katika Jiji la Dodoma.
Amesema, Kituo hicho kitatoa mafunzo mbalimbali kwa mfumo wa VETA kwa waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa wana uwezo wa kuendelea na masomo ya ufundi stadi.
Hata hivyo amesema, waraibu wanaopata matibabu katika kliniki, nyumba za uangalizi maalumu (Sober Houses), hospitali za rufaa na za kanda watapimwa maendeleo yao, na watakapobainika kuwa wamepona kwa kiwango kinachowaruhusu kujifunza, wataelekezwa katika kituo hicho cha Dodoma au kwenye vituo vingine vya VETA vilivyopo nchini.
“Ili kurahisisha mchakato huo, DCEA imeanzisha kitengo maalumu cha Social Welfare Recovery Response, ambacho jukumu lake ni kufuatilia ustawi wa waraibu waliopona, kuwaunganisha na jamii.

“Lakini pia, kuwasaidia kupata mikopo na fursa za ujasiriamali pamoja na kusimamia matumizi ya mitaji wanayopata ili kuhakikisha inaleta tija na kurejeshwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.”
Mamlaka hiyo imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha DCEA na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali za serikali.
Kamishna Lyimo amesema, hatua hiyo itasaidia kuhakikisha waraibu waliopona hawarejei tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya, huku wakipata nafasi ya kurejesha heshima yao katika jamii kupitia elimu, ujuzi na ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu VETA CPA. Athony Kasore amesema ushirikiano huo unalenga kuwapa nafasi waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa tayari kwa mafunzo, ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi.
Amesema, wahitimu watakuwa na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa au hata kuanzisha vikundi vya uzalishaji vitakavyotoa ajira kwa wengine.
Aidha, amesema makubaliano hayo yanakuja kuimarisha juhudi zilizokuwa zikifanyika awali za kuwapatia mafunzo baadhi ya waraibu waliorejeshwa kutoka DCEA.
Kupitia mfumo huo rasmi, waraibu wote watakaopokelewa watapatiwa mafunzo, kutambuliwa kwa ujuzi wao na kupewa vyeti vitakavyowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa, vyeti vitakavyotolewa vitawasaidia wahitimu kupata fursa mbalimbali za mikopo kutoka serikalini na taasisi za kifedha, hatua itakayowawezesha kuanzisha miradi na biashara za kujiongezea kipato.
CPA.Kasore ameeleza kuwa. uwekezaji katika ujuzi ni sehemu muhimu ya kuwawezesha vijana kujenga maisha bora na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma ili kukabiliana na changamoto za kijamii.
“Pia, aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi kama njia ya kujenga mustakabali wenye tija kwao na taifa,” amesema CPA. Kasore.


More Stories
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya familia
Kihongosi ahimiza ulipaji ada ya uanachama
Wadau wahimizwa kukomesha changamoto ya Taulo za kike shuleni