June 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya familia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BARNABA Mtewele mkazi wa wilaya ya Chunya mkoani hapa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama kuu ya Tanzania, kanda ya Mbeya, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwalimu wa shule ya msingi Mbugani, Herieth Lupembe (37), pamoja na Ivon Tatizo, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya sekondari Isenyela.

Mbali na mauaji hayo, mahakama pia imemtia hatiani kwa kosa la kumjeruhi mtoto Daud Barnaba Mtewele (7) katika tukio lililotokea Machi 31, 2023.

Awali, hukumu katika kesi hiyo ya jinai namba 6799/2025 ilitarajiwa kutolewa Mei 29, 2025, lakini iliahirishwa kutokana na jaji kuwa na udhuru, hivyo kupangwa upya hadi Juni 3, 2026.

Katika kesi hiyo, upande wa jamhuri uliwakilishwa na wakili wa serikali, Augustino Magesa, huku mshtakiwa akitetewa na wakili wa kujitegemea, Joyce Kasebwa.

Akitoa hukumu iliyodumu kwa saa mbili kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 11:30 jioni, Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Mbeya, Joackim Charles Tiganga, amesema ushahidi uliotolewa mahakamani ulithibitisha pasipo shaka kuwa Barnaba Mtewele alihusika na mauaji hayo pamoja na shambulio dhidi ya mtoto Daud Barnaba.

Mahakama imeelezwa kuwa Barnaba Mtewele alikuwa na mtoto mmoja na marehemu Herieth Lupembe, ambaye ni Daud Barnaba. Mtoto huyo alitoa ushahidi mahakamani akieleza kuwa baba yake alikuwa akifika mara kwa mara nyumbani kwa mama yake na siku ya tukio alimshuhudia akiwashambulia mama yake pamoja na Ivon Tatizo kwa kutumia sururu kabla naye hajashambuliwa.

Daud amedai baada ya kushambuliwa alipoteza fahamu kutokana na kuvuja damu nyingi na aliporejewa na fahamu akiwa hospitalini alimtambua baba yake mzazi kuwa ndiye aliyefanya tukio hilo.

Shahidi mwingine ambaye ni ndugu wa marehemu Herieth ameiambia mahakama kuwa mtoto huyo akiwa hospitalini alimweleza kuwa baba yake ndiye aliyewashambulia mama yake, Ivon na yeye mwenyewe.

Daktari aliyefanya uchunguzi wa miili ya marehemu Herieth Lupembe na Ivon Tatizo alieleza mahakamani kuwa vifo vyao vilisababishwa na kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha makubwa waliyopewa.

Aidha, askari wa upelelezi wa wilaya ya Chunya amesema alipokea taarifa kutoka kwa balozi wa eneo hilo baada ya jitihada za kumpata marehemu kushindikana. Amesema walipofika nyumbani walikuta milango imefungwa kwa ndani na baada ya kuivunja walikuta miili ya marehemu ikiwa na majeraha makubwa huku damu ikiwa imetapakaa eneo lote la tukio.

Polisi pia walikuta sululu iliyodaiwa kutumika kutekeleza mauaji hayo pamoja na mtoto Daud akiwa amepoteza fahamu.

Kwa upande wa utetezi, mshtakiwa amedai siku ya tukio alikuwa katika ibada ya ubatizo katika kanisa la Anglikana Chunya na aliwasilisha cheti cha ubatizo kama kielelezo. Hata hivyo, mahakama imeeleza kuwa ushahidi huo haukuthibitisha alikokuwa baada ya ibada wala haukuonyesha usajili wake katika kitabu rasmi cha kanisa.

Jaji Tiganga amesema mashahidi wa upande wa utetezi akiwemo katekista Mapunda, Joyce na Kayombo hawakuweza kuthibitisha kwa uhakika mahali alikokuwa mshtakiwa baada ya ibada hiyo.

Mahakama imesema kwa mujibu wa vifungu vya sheria vilivyotajwa, upande wa mashitaka ulifanikiwa kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa pasipo shaka yoyote.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, wakili wa serikali Augustino Magesa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria, huku upande wa utetezi ukiomba mahakama izingatie kuwa hilo lilikuwa kosa la kwanza kwa mshtakiwa.

Katika hitimisho lake, Jaji Tiganga alimhukumu Barnaba Daud Mtewele kunyongwa hadi kufa kwa makosa mawili ya mauaji ya Herieth Lupembe na Ivon Tatizo, pamoja na kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kumjeruhi Daud Barnaba.