Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema JKT itaendelea kutoa elimu ya kilimo bora, ufugaji na uvuvi kwa wananchi hata baada ya kufungwa kwa Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la JKT kwenye maonesho hayo, Meja Jenerali Mabele amesema ushiriki wa jeshi hilo katika Nanenane ni sehemu ya mkakati wa kuwafikishia wananchi maarifa, teknolojia na mbinu za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wao.
Amesema banda la JKT litaendelea kuwa kituo cha utoaji wa elimu kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani, ambapo wataalamu wa jeshi hilo wataendelea kutoa ushauri kuhusu kilimo bora, ufugaji wa kisasa na uvuvi wenye tija.
“Maonesho ya Nanenane kwetu si mwisho wa utoaji wa huduma. Tutaendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwapa elimu kuhusu mbinu bora za uzalishaji katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi,” amesema Meja Jenerali Mabele.
Ameeleza kuwa JKT imeendelea kushiriki maonesho mbalimbali nchini, ikiwemo Sabasaba na Nanenane, kwa lengo la kuwaonesha wananchi shughuli zinazotekelezwa na jeshi hilo pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mafunzo na uzalishaji.
Aidha, amesema JKT inashiriki maonesho ya Nanenane katika kanda mbalimbali nchini, zikiwemo Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa na maeneo mengine, ambako wataalamu wake wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kufanya kilimo chenye tija hata katika maeneo madogo.
Meja Jenerali Mabele amesema kupitia mafunzo hayo wananchi wanapata maarifa ya mbinu za kisasa zinazowawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha ufugaji na kuendesha shughuli za uvuvi kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa JKT imekuwa ikiboresha maonesho yake kila mwaka kwa kuzingatia maoni na ushauri wa wananchi wanaotembelea mabanda yake, ili kuhakikisha kila mwaka kunakuwa na ubunifu na maboresho yanayokidhi matarajio ya Watanzania.
“Tunataka aliyekuja mwaka jana akifika mwaka huu aone mabadiliko,tunapokea ushauri wa wananchi na kuufanyia kazi ili maonesho yetu yawe bora zaidi,” amesema.
Meja Jenerali Mabele pia amewahimiza wananchi kutembelea banda la JKT katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza teknolojia na mbinu mbalimbali za uzalishaji zinazoweza kuwasaidia kujiajiri, kuongeza kipato cha familia na kuchangia maendeleo ya Taifa

More Stories
Ndejembi:Afrika itumie gesi asilia kuharakisha upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia
Elimu ya Nishati Safi ya kupikia katika ngazi ya awali yatolewa
Serikali yaagiza usalama migodini Lindi