August 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndejembi:Afrika itumie gesi asilia kuharakisha upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi, amesema Afrika ina fursa ya kutumia rasilimali zake za gesi asilia kuharakisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi, akisisitiza kuwa rasilimali hizo zinapaswa kutumika zaidi kuchochea maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuendelea kuonekana kama bidhaa za kuuza nje pekee.

Akizungumza leo Agosti 5, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa AFRICASO na Jukwaa la Miundombinu kwa Afrika,Ndejembi amesema zaidi ya watu bilioni 2.1 duniani bado hawana huduma ya nishati safi ya kupikia, huku takribani bilioni moja wakiishi barani Afrika na asilimia 85 ya kundi hilo wakitoka katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesisitiza kuwa kufanikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia kunahitaji uwekezaji katika miundombinu ya gesi, ushirikiano wa kikanda na sera zinazowezesha upatikanaji wa nishati hiyo kwa gharama nafuu.

Ndejembi amesema kuunganishwa kwa miundombinu ya mabomba ya gesi kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Msumbiji, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutapanua upatikanaji wa LPG na CNG na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda huo.

Akielezea uzoefu wa Tanzania, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6 kabla ya mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 28 mwaka 2026, mafanikio aliyoyahusisha na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya ajenda hiyo kuwa kipaumbele cha kitaifa.

Aidha, amesema ongezeko la matumizi ya nishati safi limeongeza mahitaji ya gesi ya kupikia (LPG), ambapo uagizaji umeongezeka kutoka takribani tani 290,000 kwa mwaka hadi tani 459,000 mwaka 2025.

Hata hivyo, amesema bado kaya saba kati ya kumi nchini zinatumia mkaa na vyanzo vingine vya nishati visivyo safi kwa shughuli za kupikia.

Akihitimisha, Ndejembi amesema kufikia malengo ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030 kunahitaji dhamira ya kisiasa, ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi barani Afrika wanapata huduma hiyo muhimu.