Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanayofanyika jijini Dodoma, ambapo alipata maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati safi na teknolojia za kisasa zinazochangia maendeleo ya taifa pamoja na utunzaji wa mazingira.
Dkt. Nchimbi alitembelea banda hilo leo Juni 5, 2026 na kupokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Advera Mwijage, kuhusu mafanikio ya miradi inayotekelezwa na wakala huo katika maeneo mbalimbali ya vijijini nchini.
Akitoa maelezo hayo, Mwijage amesema REA inaonesha teknolojia mbalimbali za nishati ikiwemo matumizi ya gesi kwenye magari na bajaji, teknolojia za nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme, pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majiko banifu, umeme na gesi.
Ameeleza kuwa miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uharibifu wa mazingira na uchafuzi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira, huku ikiboresha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za maendeleo ya kiuchumi.
Mwijage amesema REA inaendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na maelekezo ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa taasisi za umma zinazohudumia zaidi ya watu 100 kuhakikisha zinatumia nishati safi ya kupikia.
“Tumefanikia shule mbalimbali kuacha matumizi ya nishati zisizo salama na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Vilevile, magereza yote nchini kwa sasa yanatumia nishati safi, hatua ambayo imechangia kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji,” amesema Mwijage.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi ya nishati safi unaendana na juhudi za Serikali za kufikia maendeleo endelevu sambamba na kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2026 yamebeba kauli mbiu isemayo: “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” inayosisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

More Stories
Wanu:Grand Challenges kukuza ubunifu Tanzania
DCEA, VETA kuwapa ujuzi warahibu dawa za kulevya
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya familia