Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mwanafalsafa wa Pan-Afrika kutoka Zimbabwe, Dkt. Joshua Maponga, amewataka Watanzania kuwa makini na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wanaharakati na wanasiasa wanaodaiwa kutumia fedha kutoka mataifa ya nje kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa makala inayochambua matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Dk. Maponga amesema Tanzania inapaswa kuendelea kulinda hadhi yake kama “Kisiwa cha Amani” kwa kuepuka ushawishi wa watu wanaochochea vurugu kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii.
“Watanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kudumisha amani. Nawasihi msiwasikilize wanaharakati na wanasiasa wanaochochea vurugu na uvunjifu wa amani kwa sababu hawana nia njema kwa taifa hili,” amesema.
Dk. Maponga amesisitiza umuhimu wa serikali kufanya tathmini na uhakiki wa kina wa baadhi ya mashirika ya kiraia ili kubaini vyanzo vya fedha wanazopokea pamoja na matumizi yake, akidai kuwa baadhi ya taasisi hizo zinaweza kuwa tishio kwa ustawi na usalama wa taifa iwapo hazitasimamiwa ipasavyo.
Ameeleza kuwa mara nyingi watu wanaohamasisha vurugu hufanya hivyo wakiwa nje ya nchi katika mazingira salama, huku wananchi wa kawaida wakibeba athari kubwa zinazotokana na machafuko hayo, ikiwemo kupoteza maisha, mali na makazi.
Katika hatua nyingine, Dk. Maponga amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya vurugu na maandamano yasiyo ya amani, akieleza kuwa matukio hayo yanaweza kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.
Makala iliyozinduliwa imeandaliwa na kampuni ya African Spear Head Media kwa lengo la kuchambua matukio yaliyotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na athari zake kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa African Spear Head Media, David Hundeyin, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi muhimu kiuchumi barani Afrika kutokana na nafasi yake ya kimkakati, hususan kupitia Bandari ya Dar es Salaam ambayo inahudumia biashara za mataifa mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kuendelea kulinda amani na rasilimali za taifa kwani machafuko yanaweza kusababisha kuyumba kwa uchumi, kupungua kwa uwekezaji na kudhoofika kwa maendeleo ya nchi.

“Vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yalikuwa na athari kubwa kwa jamii. Hata hivyo bado kuna baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu. Wananchi wanapaswa kuwa makini na watu wa aina hiyo kwa sababu hawana nia njema kwa taifa lao,” amesema Hundeyin.
Ameongeza kuwa amani, umoja na utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, hivyo kila Mtanzania anapaswa kushiriki kikamilifu katika kuvilinda na kuvienzi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

More Stories
Nchimbi ashuhudia mchango wa nishati safi,aipongeza REA
Wanu:Grand Challenges kukuza ubunifu Tanzania
DCEA, VETA kuwapa ujuzi warahibu dawa za kulevya